• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
TAHARIRI: Utoaji magari kwa MCAs ufuate sheria

TAHARIRI: Utoaji magari kwa MCAs ufuate sheria

KITENGO CHA UHARIRI

MDHIBITI wa Bajeti Jumapili alipiga breki utekelezaji wa ahadi ya Rais Uhuru Kenyatta kwa madiwani ya kuwapatia Sh2 milioni kila mmoja za kununua magari kwa kupitisha Mswada wa Mabadiliko ya Katiba, almaarufu BBI.

Naibu Mdhibiti wa Bajeti Stephen Masha alisema kwamba itakuwa vigumu kutimiza ahadi hiyo huku akisema kuwa wamebaini kuna dosari katika utekelezwaji wake.

Ni habari ambayo bila shaka itawavunja moyo madiwani wengi ambao wamekuwa wakishangilia na kusubiri kwa hamu magari hayo lakini pia itakuwa afueni kwa Wakenya wengi wanaokosoa mpango huo haswa katika kipindi hiki cha matatizo makubwa ya kiuchumi.

Tangu Rais Kenyatta atangaze ruzuku hiyo, malumbano yametanda kila kona. Wengi wanashangaa iweje kwa serikali ambayo inashindwa kulipa wahudumu wa afya iweze kutoa zawadi ya magari kwa wanasiasa ambao tayari machoni pa wengi wana mishahara na marupurupu mengi. Zaidi lililokoroga wengi nyongo ni kubaini kwamba zawadi hiyo inatolewa kama ‘hongo’ hivi kwa watunga sheria hao wa Kaunti kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba ambao tayari unapingwa na sehemu ya wananchi. Mashirika ya kijamii na wanasiasa kadhaa hawaungi mkono mabadiliko hayo ambayo yatapelekea kufanyika kwa refarenda kabla ya kuisha kwa mwaka huu.

Mashirika hayo na wanaopinga mpango huo walitegemea kwamba Tume ya Mishahara na Marupurupu SRC itatupilia mbali ruzuku hiyo iliyo na thamani ya jumla ya Sh4.5 bilioni, lakini badala yake tume hiyo ilithibitisha kwamba itageuza mikopo ya magari ya Sh4.5 bilioni kuwa pesa za bwerere kwa madiwani hao.

Lakini sasa Afisi ya Mdhibiti wa Bajeti imejitokeza kusema sheria haijafuatwa katika utoaji wa ruzuku hiyo na kwamba utekelezwaji wake hautawezekana. Ingawa dalili zote zinaonekana kwamba serikali imeaminia kutoa ruzuku hiyo licha ya pingamizi, kile ambacho wengi wanatarajia ni kwamba angalau basi sheria ifuatwe katika utekelezwaji wake. Kwa hili, serikali nayo haijakuwa na rekodi nzuri ya kufuata sheria na maagizo ya afisi huru huku kumbukumbu ya kisa cha wakili Miguna Miguna kufurushwa nchini licha ya maagizo ya mahakama kuharamisha kufushwa kwake ikiwa akilini mwa wengi.

Labda pingamizi hii mpya ya ruzuku hii ni dalili nyingine kwa serikali kufikiria upya kuhusu hatua hii. Kuona kwamba taifa lina matatizo mengi na ya dharura zaidi. Kwamba pesa hizo zinahitajika kwa Wakenya wengi ambao hata hawana uwezo wa kumudu mlo wa siku.

You can share this post!

WARUI: Kazi kwenu sasa Jwan, Ruto kufanikisha mfumo wa CBC

Ndumba yazima uchu wa jombi