Ndumba yazima uchu wa jombi

Na JOHN MUSYOKI

KABATI, KITUI

KALAMENI mwenye tamaa ya kunyemelea wake wa wanaume wengine aliwachekesha wenzake nusra wavunjike mbavu alipowaeleza jinsi alivyotishika alipomuona mume wa mwanamke aliyekuwa akichepuka naye akitoka nyumba ya mganga.

Kalameni alikuwa na mazoea ya kuchepuka na mke wa mtu na licha ya kuonywa hakubanduka.

Mume wa mwanamke huyo alikuwa amemuonya na hata kumtumia wazee lakini kalameni akapuuza na kumwambia waziwazi kuwa iwapo alikuwa hamkolezi mkewe uroda, hakuwa na budi kumsaidia.

“Bwana wee, mke wa mtu huchezewa na mwanamume asiyetaka kuishi. Iwapo huyathamini maisha yako, endelea kuchezea mke wangu,” mume alimwonya.

“Kama ungekuwa ukimpa anachokikosa, asingenitafuta. Nitaendelea kumlevya kwa mahaba maanake ananipenda,” kalameni alisema.

“Haina tabu. Endelea kufanya ufanyalo utajua hujui, ” mume alimwonya kwa mara ya mwisho, hasira za mkizi zikimpanda.

Juzi aliwasiliana na mke wa jamaa na wakapanga wakutanie mahali fulani mjini. Walitembea kuelekea lojing’i moja lakini kabla ya kufika, walipomuona mume wa demu akitoka nyumba ya mganga maarufu.

“Hebu mtazame mumeo. Nionavyo ameamua kunimaliza,” kalameni alimwonesha demu sehemu aliyosimama mumewe na mganga.

“Kweli yule ni mume wangu. Kitu gani ameshikilia mkononi?”

“Zile ni ndumba za kutufunga. Unakumbuka mganga huyu ndiye aliyewafanya jamaa mwengine na mke wa mtu kukwama wakifanya ufuska?” kalameni aliuliza alitetemeka.

“Una woga mwingi bwana. Twende unikate kiu ya mahaba,” demu alirai.

“Siwezi kuunyanyua mguu wangu. Sitaki aibu itakayotazamwa na ulimwengu katika runinga na kusikika redioni. Sitaki kula nyasi mie,” kalameni alieleza akigeuka kuondoka.

“Sina hamu. Imeniisha kabisa. Afadhali tusitishe haya tuyafanyayo mafichoni. Natamani kuiona kesho,” kalameni alisema akieleza wenzake aliondoka na kumwacha demu akizubaa.