• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:55 PM
DIMBA: Josh ‘magic’ Maja: Fimbo ya Fulham iliyosagasaga Everton

DIMBA: Josh ‘magic’ Maja: Fimbo ya Fulham iliyosagasaga Everton

Na GEOFFREY ANENE

KINDA Josh Maja alitangaza kuwasili kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kishindo yapata wiki moja iliyopita.

Aliibuka shujaa wa Fulham ikizamisha wenyeji Everton, wanaonolewa na mkali wao Carlo Ancelotti, kwa mabao 2-0 mnamo Februari 14.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Maja kuanza mechi tangu kocha Scott Parker amnunue kutoka Bordeaux hapo Februari 1.

Mabao yake yaliwezesha Fulham kuandikisha ushindi wa kwanza ligini tangu Novemba 2020 ilipopepeta Leicester 2-1.

Fulham wako katika mduara hatari wa kushushwa ngazi mwisho wa msimu – timu tatu za mwisho hubanduliwa EPL na kutupwa ligi ndogo ya Championship.

Ushindi dhidi ya Everton uliwapa motisha ya kujituma zaidi, wakajikakamua katikati ya wiki na kutoka sare ya 1-1 na Burnley.

Maja na wenzake hawakukoma hapo; Jumamosi waliongeza bidii na kufaulu kubamiza wanyonge wenzao Sheffield United 1-0.

Ni ushindi uliowazidishia alama hadi 22 na kupanua mwanya kati yao na wanyonge wenzao West Brom (14) na Sheffield (11), huku zikiwa zimesalia mechi 13 msimu kutamatika.

Je, Maja na wenzake wataweza kuokoa timu kufikia mwisho wa msimu?

Mshambuliaji huyo alizaliwa jijini London, Uingereza, mnamo Desemba 27 mwaka 1998.

Josh Magic, anavyofahamika kwa jina la utani, ana asili ya Nigeria na anatoka katika familia inayojiweza.

Uchezaji wake wa soka ulianza kupata mwelekeo alipofanya majaribio na klabu za Crystal Palace na Fulham na kupita.

Ili kuimarisha uchezaji wake nje ya jiji la London, Maja alihama Fulham na kujaribu bahati katika akademia ya Manchester City.

Alitandaza kabumbu yake katika akademia hiyo iliyokuwa na nyota wa sasa wa Dortmund, Jadon Sancho.

Alikuwa na matumaini City itampa ufadhili. Hata hivyo, mabwanyenye hao hawakuwa makini kutimiza hilo, hivyo Josh aliondoka mnamo 2015 na kuelekea Sunderland – umbali wa kilomita 218 kutoka Manchester.

Hapa, Maja alifaulu kupata ufadhili wa miaka miwili. Alipiga hatua nyingine muhimu Mei 2016 aliposaini kandarasi ya kwanza ya soka ya malipo. Ilikuwa ya miaka mitatu.

Miezi mitano baadaye, Maja alipata kuchezea ‘Black Cats’ walipoamua kumtumia dhidi ya Queens Park Rangers katika kombe dogo la League Cup.

Alijaza nafasi ya Joel Asoro zikisalia dakika 21 katika mechi ambayo Sunderland iling’aria QPR 2-1.

Straika hiyo aliishia kupasha benchi moto msimu huo wa 2016-2017 kwani hakutumiwa tena.

Timu yake ilishushwa daraja mwisho wa msimu hadi ligi ya Championship, hatua iliyomfungulia Maja mlango wa kutumiwa zaidi ligini.

Mnamo Desemba 2017, aliingia kama mchezaji wa akiba na kupachika bao la pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya timu yake ya zamani Fulham.

Alishiriki michuano mingine 16 kwenye ligi hiyo ya daraja ya pili, ingawa hakuchana nyavu tena timu ikiangukiwa na shoka tena hadi daraja ya tatu.

Kutemwa kwa Sunderland kwa mara ya pili mfululizo kulikuwa baraka kwa Maja kwani alipata namba ya kuanza mechi za Sunderland.

Aliifungia mabao katika michuano minne ya kwanza Agosti 2018 na kuteuliwa mchezaji bora wa klabu mwezi huo.

Fursa ya kuongeza kandarasi yake klabuni Sunderland ilijitokeza, lakini akaikataa akimezewa mate na klabu kadhaa.

Aliondoka uwanjani Stadium of Light akiwa amefungia Sunderland mabao 16 katika mechi 30, na kujiunga na Bordeaux ya Ufaransa kwa kandarasi ya miaka minne na nusu mnamo Januari 2019.

Wiki chache baadaye, alianza maisha Bordeaux kwa kichapo cha 2-1 akichezeshwa dakika 67 za kwanza dhidi ya Toulouse. Ingawa hivyo, alipata bao lake la kwanza katika mechi hiyo.

Pigo lingine likampata alipojeruhiwa goti la kushoto katika kipindi cha kwanza dhidi ya Nimes mnamo Aprili 20. Akakamilisha msimu huo kwa kuchezea Bordeaux michuano saba pekee.

Josh Magic alirejea ulingoni tena Oktoba 2019 na kupata ‘hat-trick’ yake ya kwanza kabisa katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Nimes miezi mitatu baadaye.

Josh Magic alikamilisha msimu huo wa 2019-2020 akiwa amechezea Bordeaux michuano 24 katika mashindano yote, na kuifungia mabao manane.

Akachezea mechi zingine 17 na kufunga magoli mawili kabla kurejea ‘nyumbani’ Fulham kwa mkopo wa miezi mitano hapo Februari 1 mwaka huu.

Akadhihirisha ukali wake kwa kufungia Fulham mabao yote mawili ikipepeta 2-0 uwanjani Goodison Park wiki iliyopita.

Fulham wanatumai makali ya Josh Magic yatawasaidia kujikomboa kutoka minyororo ya kushushwa daraja.

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Nigeria, almaarufu Super Eagles, alikuwa akipokea mshahara wa Sh1.9 milioni kila wiki Bordeaux. Ana ndugu watatu na dada mmoja.

You can share this post!

Ndumba yazima uchu wa jombi

UDAKU: Mke wa zamani wa Mahrez ameamua kuuza picha za uchi