Kenya Morans kurejea nchini wiki hii baada ya kupiga miamba Angola na kufuzu kushiriki AfroBasket 2021

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya mpira wa vikapu ya wanaume ya Kenya almaarufu Morans, itarejea nchini usiku wa kuamkia Jumatano kutoka Cameroon ilikoandikisha historia kupiga miamba Angola na kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AfroBasket) 2021.

Morans, ambayo inanolewa na raia wa Australia Elizabeth Mills, imeingia katika AfroBasket kwa mara ya kwanza tangu 1993 ikifungia nje Msumbiji ambayo ilikuwa imeshiriki makala 10 mfululizo yaliyopita.

Wakenya walimaliza Kundi B katika nafasi ya tatu kwa alama nane. Walipata tiketi baada ya kuduwaza mabingwa mara 11 Angola 74-73 mnamo Februari 20 na kulemea Msumbiji 79-62 mnamo Novemba 27, 2020.

Morans walipoteza michuano yote dhidi ya Senegal 92-54 (Novemba 25,2020) na 69-51 (Februari 19,2021), kulimwa na Angola 75-52 (Novemba 26) na kunyamazishwa 71-44 mikononi mwa Msumbiji katika siku ya mwisho ya kufuzu Februari 21.

Mbali na Kenya, timu nyingine zilizojikatia tiketi ya kushiriki dimba la AfroBasket kutoka Ukanda wa tano (Zone 5) ni Misri (washindi Kundi E), Rwanda (wenyeji) na Sudan Kusini (nambari mbili Kundi D). Uganda pia inapigiwa upatu kufuzu kutoka Kundi E. Mechi za Uganda dhidi ya Misri (Ferbruari 18), Morocco (Februari 20) na Cape Verde (Februari 21) hazikuendelea jinsi ilivyopangwa baada ya kambi ya Uganda kuwa na visa vitano vya maambukizi ya virusi vya corona. Tarehe mpya ya mechi hizo bado haijatangazwa.

Timu nyingi zilizofuzu ni Nigeria na Mali (Kundi D), Senegal na Angola (Kundi B), Ivory Coast na Cameroon (Kundi C), Tunisia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Kundi A). Nafasi tatu zimesalia idadi ya washiriki wa 2021 AfroBasket ikamilike. Wawili kutoka orodha ya Cape Verde, Morocco na Uganda watafuzu kutoka Kundi E pamoja na mmoja kati ya Guinea na Equatorial Guinea kutoka Kundi C.