Maangi apinga madai kupanga baadhi ya viongozi wazomewe katika mazishi ya Mzee Nyachae

Na SAMMY WAWERU

NAIBU Gavana wa Kisii Bw Joash Maangi amejitetea vikali kuhusu kukamatwa kwake wakati wa mazishi ya Mzee Simeon Nyachae mnamo Februari 15, 2021.

Bw Maangi pamoja na mbunge wa Mugirango Kusini, Silvanus Osoro walitiwa nguvuni na maafisa wa polisi kwa tuhuma za kupanga baadhi ya viongozi wazomewe katika mazishi ya Mzee Nyachae, ambayo yalihudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, miongoni mwa viongozi wengine wakuu serikalini na wanasiasa.

Waziri huyo wa zamani alizikwa katika kijiji cha Nyosia, Kaunti ya Kisii, na Mabw Maangi na Osoro waliachiliwa huru baada ya hafla ya kumpa heshima za mwisho mwendazake kukamilika.

Aidha, Bw Maangi amesema Jumatatu kukamatwa kwake hakukuwa na msingi wowote ule.

Naibu Gavana huyo ametaja madai kuwa alipanga kuchochea baadhi ya viongozi wazomewe katika mazishi ya Mzee Nyachae, kama chochezi za kisiasa.

“Bw Charles Nyachae (mwanawe Mzee Nyachae) ni rafiki yangu wa karibu. Kwa vyovyote vile isingewezekana nichochee mazishi ya Mzee wetu yatatizwe. Hayo yalikuwa madai potovu ya kisiasa,” Bw Maangi akasema.

Alisema kilichosababisha kukamatwa kwake ni kujiandaa kumlaki Naibu wa Rais, Dkt Ruto katika uga wa Gusii (ambao Rais Kenyatta aliubadilisha jina na sasa unatambulika kama Simeon Nyachae Stadium), ambapo umati mkubwa ulimsubiri.

“Walioeneza tetesi kwamba nilikuwa na mipango kuchochea fujo zizuke, hawakuridhishwa na idadi ya juu ya watu waliojitokeza kumkaribisha Naibu wa Rais. Nilikuwa katika uga huo kumlaki, ana ufuasi mkubwa Kisii,” akasema mwandani huyo wa Dkt Ruto.

Mnamo Februari 1, 2021, katika mazishi ya babake Maangi, Mzee Abel Gongera, mbunge Osoro na mwenzake wa Dagoretti, Simba Arati waliangushiana makonde hadharani.

Wawili hao walitwangana mbele ya Naibu wa Rais, Dkt William Ruto na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kitendo ambacho kilikashifiwa vikali na kutajwa kama cha aibu.