AUSTRALIAN OPEN: Djokovic atwaa taji la tisa na kuendeleza ubabe kwenye ulingo wa tenisi
Na MASHIRIKA
MWANATENISI Novak Djokovic aliendeleza umahiri wake kwenye mchezo huo kwa kumbwaga Daniil Medvedev kwenye mechi ya Australian Open na hivyo kutia kapuni taji lake la tisa.
Djokovic, 33, alimcharaza Medvedev 7-5, 6-2, 6-2 na kutwaa ufalme wa 18 wa Grand Slam, ufanisi unaomsaza na mataji mawili zaidi kuwafikia miamba wa dunia Roger Federer na Rafael Nadal.
Nyota huyo raia wa Serbia anayenolewa na kocha Goran Ivanisevic, hajawahi kupoteza mechi yoyote ya Australia Open ugani Melbourne Park na ushindi wake dhidi ya Medvedev ulikuwa wa tatu mfululizo.

Medvedev, 25, sasa amepoteza fainali mbili za kuwania ubingwa wa Grand Slam. Mchezaji huyo raia wa Urusi alizidiwa maarifa na Nadal kwenye fainali ya US Open jijini New York mnamo 2019 na alijibwaga ugani kuvaana na Djokovic akipigiwa upatu wa kutia kapuni taji lake la kwanza la Grand Slam.
Medvedev alifuzu kwa fainali baada ya kupepeta Stefanos Tsitsipas wa Ugiriki kwa seti 3-0 za (6-4, 6-2, 7-5) kwenye Australian Open mnamo Jumamosi. Ushindi huo, uliokuwa wake wa 20 mfululizo, ulimkatia tiketi ya fainali ambapo alitarajiwa kuweka historia ya kuwa mwanatenisi wa kwanza raia wa Urusi tangu 2005 kuwahi kutwaa ufalme wa Grand Slam.
Japo Medvedev aliwahi kumshinda Djokovic mara tatu katika michuano minne ya awali, mechi ya Jumapili kwenye fainali ilitawaliwa na ushindani mkali ikizingatiwa kwamba nyota huyo raia wa Serbia hakuwahi kupoteza pambano lolote la fainali ya Australian Open.
Sawa na Djokovic, Medvedev naye anafahamika zaidi kwa ukali wa mipakuo yake na fataki yake moja ina uwezo wa kufikia umbali wa kilomita 216 chini ya kipindi cha dakika 60.
Bingwa huyo mtetezi wa ATP Finals alimcharaza Tsitsipas, 22, kirahisi na kusajili ushindi wake wa 12 mfululizo dhidi ya mpinzani aliye katika orodha ya wanatenisi 10-bora duniani. Rekodi ya kutoshindwa kwa Medvedev katika jumla ya mechi 20 kabla ya fainali ya Australia Open ilianzia jijini Paris, Ufaransa mnamo Novemba 4, 2020.
Tangu wakati huo, alifaulu kuwapiku Djokovic, Nadal na Dominic Thiem miongoni mwa wanatenisi wanaoshikilia orodha ya 10-bora kimataifa.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO