Simba aua mbuzi na kondoo katika vijiji kadhaa Lamu

Na KALUME KAZUNGU

TAHARUKI imetanda kwenye vijiji vya Tewe, Swabaha, Lake Amu na Baharini, tarafa ya Mpeketoni, Kaunti ya Lamu baada ya simba kuvamia na kuua zaidi ya mbuzi na kondoo 10 eneo hilo.

Wakazi waliozungumza na Taifa Leo wamesema simba huyo anaaminika kutoka kwenye mbuga ya wanyama ya Boni Dodori ili kujitafutia mawindo rahisi kwenye makazi ya binadamu.

Wakazi pia wamelalamikia ongezeko la nyati ambao wamekuwa wakirandaranda ovyo mitaani kwenye vijiji hivyo hasa tangu msimu wa kiangazi ulipoanza mapema mwaka 2021.

Kulingana na mmoja wa wakulima wa eneo la Baharini, Bw Kimani Wanyoike, wakazi wamekuwa wakilazimika kulala kwenye mazizi wakilinda mifugo yao usiku ili wasiuawe na kuliwa na simba.

“Mbuzi na kondoo kadhaa wameliwa na simba aliyevamia makazi ya binadamu katika vijiji vya hapa tangu wiki jana hivyo tunaomba Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) kutusaidia kumfurusha mnyama huyo anayetusababishia hasara,” akasema Bw Wanyoike.

Naye mwathiriwa Bw John Mugo aliyegongwa na kuumizwa sehemu moja ya kichwa chake na nyati ameomba KWS ifanye jinsi iwezavyo kuwafurusha na kuwarudisha nyati msituni walikotoka mbali na makazi ya binadamu.

Bw Mugo pia ameiomba serikali kupitia KWS kuwafidia waathiriwa ambao mifugo yao imeliwa na simba au wale ambao wamejeruhiwa na nyati.

“Wawafurushe hawa wanyama. Hawatupi amani. Isitoshe, wafikirie kutufidia sisi ambao tumeumizwa na nyati au mifugo wetu kuliwa na simba,” akasema Bw Mugo.

Akirejelea suala hilo, Kamanda wa KWS Kaunti ya Lamu, Mathias Mwavita amesema bado hawajapokea ripoti zozote kuhusu simba wanaorandaranda mitaani Lamu.

Alisema ripoti iliyofikia ofisi yake ni ile ya nyati ambao wamekuwa wakionekana mitaani n ahata kuvamia wananchi, hasa kwenye maeneo ya Wit una Mkunumbi.

Bw Mwavita aidha alisema atafuatilia malalamishi hayo ya kuwepo kwa simba kwenye makazi ya binadamu kuitatua.

“Tumepokea ripoti nyingi za nyati kuvamia makazi ya binadamu eneo la Lamu msimu huu wa kiangazi. Hata tumefaulu kuua nyati wawili baada ya kujaribu kuvamia maafisa wetu huko Wit una Mkunumbi. Kilio cha simba sijajulishwa lakini nitafuatilia na kuhakikisha simba husika wanafurushwa kwenye makazi ya watu,” akasema Bw Mwavita.

Mnamo Juni, 2020, maagfisa wa KWS walimkamata simba aliyekuwa akiua mifugo na kuhangaisha wakazi eneo la Lake Amu huko Lamu.

Habari zinazohusiana na hii