Leicester City wana kila sababu ya kumaliza kampeni za EPL ndani ya mduara wa 4-bora msimu huu – Brendan Rodgers

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Brendan Rodgers wa Leicester City amesema kwamba kikosi chake kinajivunia utulivu mkubwa kadri kinavyozidi kufukuzia nafasi ya kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Leicester waliwacharaza Aston Villa 2-1 mnamo Jumapili na kufungua pengo la alama nne kati yao na nambari nne West Ham United. Ushindi huo uliwadumisha masogora wa kocha Rodgers katika nafasi ya tatu kwa alama 49 sawa na Manchester United wanaowazidi kwa wingi wa mabao.

Mabao ya Leicester katika mechi iliyowakutanisha na Villa yalifumwa wavuni na James Maddison na Harvey Barnes huku wenyeji wakifungiwa na Bertrand Traore.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu Oktoba 1960 kwa Leicester kushinda Aston Villa katika mechi mbili mfululizo za EPL.

Katika kampeni za msimu wa 2019-20, Leicester walikosa fursa kufuzu kwa soka ya UEFA baada ya kupokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Man-United katika siku ya mwisho ya muhula huo licha ya kudumu ndani ya mduara wa nne-bora kwa kipindi kirefu.

“Matukio hayo ya mwisho wa msimu uliopita wa 2019-20 yalituweka katika ulazima wa kutathmini matokeo yetu kila baada ya kipindi kifupi. Kwa sasa tuna utulivu mkubwa na kikosi kinacheza soka ya kuvutia,” akasema kocha huyo wa zamani wa Liverpool.

Maddison, 24, kwa sasa amehusika moja kwa moja katika mabao manane ambayo yamefungwa na Leicester kutokana na mechi tisa zilizopita ligini. Ufufuo wa makali yake kambini mwa Leicester ni miongoni mwa masuala ambayo yanamfanya kupigiwa upatu wa kuunga kikosi cha Uingereza katika mechi tatu zijazo za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Aston Villa kwa sasa wanajiandaa kupepetana na Leeds United katika mchuano wao ujao wa EPL mnamo Februari 27. Kwa upande wao, Leicester watakuwa wenyeji wa Slavia Prague ya Jamhuri ya Czech katika mchuano wa mkondo wa pili wa Europa League mnamo Februari 25, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Habari zinazohusiana na hii