Watatu waangamia baada ya matatu kupoteza mwelekeo na kubingiria Makueni

Na PIUS MAUNDU

WATU watatu walifariki mnamo wikendi baada ya matatu walimokuwa kubingiria katika eneo la Mbuvo, barabara ya Wote-Makindu, Kaunti ya Makueni.

Wanne walionusurika, walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Makueni kupata matibabu.

Kulingana na walioshuhudia, dereva wa matatu alipoteza mwelekeo baada ya gurudumu kupasuka alipokuwa akijaribu kupita gari lililokuwa mbele yake.

Gari hilo lilikuwa likielekea Mjini Makindu, na walioshuhudia walieleza kwamba liliondoka barabarani na kubingiria.

“Matatu hiyo ilipoteza mwelekeo baada ya gurudumu kupasuka wakati dereva akijaribu kupita gari lililokuwa mbele yake,” akasema mmoja wa walioshuhudia.

Aidha, walioshuhudia ajali hiyo walisema matatu hiyo ilikuwa imebeba abiria 16 badala ya 14.

Sheria na mikakati kusaidia kudhibiti Covid-19 katika sekta usafiri na uchukuzi imependekeza magari ya uchukuzi wa umma kubeba asilimia 60 ya idadi jumla.

Miili ya walioangamia ilipelekwa katika Hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Makueni.

TAFSIRI: Sammy Waweru