WHO yataka serikali ya Tanzania ifichue takwimu za corona

Na MASHIRIKA

DAR ES SALAAM, Tanzania

RAIS Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kuvaa barakoa katika vita dhidi ya ugonjwa wa corona.

Hata hivyo, Magufuli amewatahadharisha Watanzania dhidi ya kuvaa barakoa zinazotoka nje ya nchi bali kutumia zinazoundwa nchini humo au zilizopendekezwa na wizara ya afya na wataalamu wa utabibu.

Katika uzi huo huo, shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa wito kwa serikali ya Tanzania kufichua data ya COVID-19 na kutekeleza mikakati kuhusu afya ya umma ili kukomesha misururu ya maambukizi ya virusi hivyo hatari.

Taarifa kutoka kwa kiongozi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus mnamo Jumamosi ilisema kuwa Tanzania bado haijatoa habari kuhusu mikakati iliyochukua dhidi ya janga hilo.

“Hali imesalia kuwa ya wasiwasi mno. Ninatoa wito kwa mara nyingine kwa Tanzania kuanza kuripoti visa vya Covid-19 na kutangaza data,” ilisema taarifa hiyo.

Taifa hilo la Afrika Mashariki lilitoa data kwa mara ya mwisho kuhusu COVID-19 mnamo Mei 2020, wakati Rais John Magufuli alipohoji ufaafu wa vifaa vya vipimo vilivyoagizwa kutoka mataifa ya kigeni.

Tanzania imepuuzilia mbali matibabu yote ya kisasa na imekuwa ikipigia debe matumizi ya michanganyiko ya dawa za mitishamba kupambana na virusi hivyo.

 

Habari zinazohusiana na hii