Bobi Wine sasa ainua mikono, amwachia Mungu

Na LEONARD ONYANGO

KIONGOZI wa Chama cha National Unity Platform (NUP) nchini Uganda, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, ameondoa kesi aliyowasilisha katika Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya urais ya uchaguzi mkuu uliopita ambapo Rais Yoweri Museveni aliibuka mshindi.

Bobi Wine aliyekuwa akizungumza Jumatatu jijini Kampala alisema kwamba, baadhi ya majaji wa Mahakama ya Juu wanaonekana kuegemea upande wa Rais Museveni hivyo uwezekano wa kupata haki ulikuwa mdogo.

“Tumeondoa kesi mahakamani lakini hatutatumia fujo kudai haki. Tumejitoa kwenye korti ya Owiny Dollo (Jaji Mkuu),” akasema Wine.

Hatua hiyo inafuatia siku moja baada ya Rais Museveni, Tume ya Uchaguzi na Mkuu wa Sheria kuwasilisha stakabadhi zao za kujibu vigezo 53 ambavyo mawakili wa chama cha NUP waliwasilisha kortini kuthibitisha kwamba, uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 14 haukuwa huru na wa haki.

Wakili wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) Jumapili alisema Bobi Wine atawalipa kiasi kikubwa cha fedha endapo angeondoa kesi hiyo katika Mahakama ya Juu.

Mkurugenzi wa Idara ya Sheria ya NRM aliambia wanahabari kuwa, watamtaka Bobi Wine kuwalipa fedha walizotumia kujiandaa kujibu mashtaka aliyowasilisha kortini kupinga ushindi wa Rais Museveni.

Lakini Anthony Wameli, mmoja wa mawakili wa Bobi Wine, alisema kuwa wako tayari kulipa gharama zote baada ya kuondoa kesi hiyo mahakamani.

“Tunafahamu kuwa kuondoa kesi kortini huandamana na gharama. Sidhani kwamba mteja wangu atashindwa kulipa fedha hizo,” akasema Wameli.

“Hatuna tatizo na kulipa gharama kwa sababu tangu tulipoamua kuwa tunaenda kupinga matokeo ya uchaguzi tumetumia kiasi kikubwa cha fedha,” akaongezea.

Jaji Mkuu Alfonse Owiny-Dollo na majaji wengine wawili wa Mahakama ya Juu, wiki iliyopita walikataa ombi la Bobi Wine la kuwataka kujiondoa kwenye jopo la majaji ambao wangesikiliza kesi hiyo.

Museveni, 76, ambaye alianza kuongoza Uganda mnamo 1986, alishinda muhula wa sita baada ya kupata asilimia 59 ya kura zilizopigwa. Bobi Wine alifuatia kwa asilimia 35.

Msemaji wa Idara ya Mahakama Solomon Muyita, Jumatatu alisema kuwa, Bobi Wine hajawasilisha ombi rasmi kortini kutaka kuondoa kesi hiyo.

“Alichosema (Bobi Wine) ni tamko la kisiasa lakini kufikia sasa mawakili wake hawajawasilisha ombi rasmi kortini kwamba anataka kuondoa kesi,” akasema Muyita.

Kuondolewa kwa kesi hiyo kunamaanisha kuwa Rais Museveni yuko huru kuapishwa kuongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa miaka mitano ijayo.