Raila akausha marafiki

Na WANDERI KAMAU

VIGOGO wa Muungano wa NASA Jumatatu waliendelea kurushiana cheche za maneno kuhusu madai ya ‘usaliti’ kwenye hafla tata ya kumwapisha kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kama “rais wa wananchi” mnamo Januari 30, 2018.

Jinamizi hilo linaibuka upya miaka mitatu baada ya kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula kususia hafla hiyo katika hali tatanishi.

Mnamo Jumamosi, Bw Odinga alisema hataweza kuwaunga mkono vigogo wenzake kuwania urais 2022, akiwataja kama “waoga” baada yao kukosa kuhudhuria hafla hiyo.

Bw Odinga alisema watatu hao walimwacha wakati aliwahitaji zaidi. Hata hivyo vinara wenza walimkemea kiongozi huyo wa upinzani wakisema ametupa kapuni muafaka wa kuunga mmoja wao kuwania urais 2022.

Akihutubia wakazi wa Ndhiwa, Homa Bay mwishoni mwa juma, Bw Odinga alisema: “Wakati tulikuwa tukienda kwenye hafla ya kuniapisha, walikataa. Walizima simu zao na walikuwa wakitetemeka kutokana na wasiwasi. Sasa wanataka niwaunge mkono. Siwezi kuwaunga mkono kwani walionyesha uoga wao,” akasema Bw Odinga, alipohutubu katika eneo la Ndhiwa.

Jumatatu, Bw Odinga alielezea kwa kina mikakati waliokuwa wameweka kuhakikisha kila mmoja amefika katika uwanja huo, kwa kukwepa vikwazo vya kiusalama ambavyo walikuwa wamewekewa na serikali.

“Kabla ya hafla yenyewe, NASA iliandaa msururu wa mikutano iliyoitwa ‘jukwaa la wananchi.’ Mkutano wa mwisho ulifanyika Homa Bay, ambapo Bw Mudavadi alitoa hakikisho kwamba hakuna lolote ambalo lingeusimamisha mpango huo. Bw Musyoka hata alisema alikuwa tayari kumwapisha Bw Odinga Homa Bay, hata kabla ya mkutano wa Uhuru Park,” akasema, kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na mwenyekiti wa ODM, John Badi.

Bw Odinga aliwalaumu watatu hao kwa kutoa visingizio kuhusu sababu ambapo hawakufika, licha yao kuweka mipango kabambe kuhusu vile kila mmoja angeweza kufika kwenye hafla.

Ilibainika Bw Odinga alikuwa ameahidi kuwapigia simu kwa kutumia laini kutoka Nigeria.

“Baadaye, walidai walikosa kufika haflani kwani serikali iliwazuilia majumbani mwao. Serikali ilikanusha madai hayo. Tulifahamu watatu hao walipanga njama na serikali wakamatwe ili watoe visingizio kuhusu sababu ambapo hawakuweza kufika,” akadai Bw Odinga.

Jumapili, Bw Musyoka alisema hangeweza kushiriki kwenye hafla hiyo kwani ilikuwa kinyume cha sheria.

Jumatatu, Bw Musyoka alimtaja Bw Odinga kuwa kiongozi msaliti, ambaye hawezi kutegemewa na wenzake.

“Ni wazi kuwa Bw Odinga amekuwa akiwasaliti waandani wake wa kisiasa bila kujali,” akasema Bw Musyoka.

Alirejelea ‘usaliti’ huo kutokea tangu Bw Odinga alipoungana na Kanu mnamo 2001 kupitia chama chake cha NDP, kundi la ‘Pentagon’ kwenye uchaguzi wa 2007/2008, muungano wa Cord na Nasa.

“Kwa mwelekeo huo, si ajabu ikiwa Bw Odinga atamwacha Rais Uhuru Kenyatta na kuungana na wapinzani wake ielekeapo 2022 ili kutimiza malengo yake,” akasema Bw Musyoka.

Sawa na Bw Musyoka, Bw Mudavadi alimtaja Raila kuwa “mdanganyifu.”

Kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Kibisu Kabatesi, Bw Mudavadi alisema mnamo 2017, Bw Odinga aliwadanganya hatawania tena urais ikiwa wangeshinda au la.

“Pengine uoga wetu ni kumruhusu Raila kutudanganya,” akasema Bw Mudavadi.

Kutokana na mielekeo hiyo, wadadisi wanasema makabiliano zaidi yatashuhudiwa, ikizingatiwa vigogo hao wote wametangaza azma za kuwania urais 2022.

Ingawa bado hajatangaza iwapo atawania urais, Bw Odinga anategemea handisheki kati yake na Rais Kenyatta kupiga jeki juhudi zake.

Mabwana Musyoka, Mudavadi na Wetang’ula wametangaza muungano wa kisiasa na Seneta Gideon Moi (Baringo) ambaye ndiye kiongozi wa Kanu.

Habari zinazohusiana na hii

UHURU AMTULIZA RAILA