Kidero akemea wanaovuruga mikutano

Na GEORGE ODIWUOR

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero na Mbunge wa Rangwe Dkt Lilian Gogo wamewakashifu baadhi ya viongozi wa Kaunti ya Homa Bay kwa kutumia vijana kuvuruga mikutano ya wapinzani wao.

Wawili hao wamesema tabia ya kuwatuma vijana ili kuwazomea viongozi katika mikutano ya kisiasa na hafla za mazishi inakera na itahujumu amani katika kaunti hiyo.

Kampeni za kiti cha ugavana tayari zimeshika kasi katika kaunti hiyo huku ukisalia mwaka moja na nusu kabla ya kura ya 2022.

Kando na Dkt Kidero, wengine wanaomezea mate kiti hicho ni Mwenyekiti wa ODM John Mbadi, aliyekuwa mbunge wa Kasipul Oyugi Magwanga, Katibu wa kaunti Isaiah Ogwe na Mbunge Mwakilishi wa wanawake Gladys Wanga.

Wengine ni Naibu Gavana Hamilton Orata, Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori na Mfanyabishara Jared Kiasa.

“Kuna wanasiasa ambao wanakutusi ukiwa mikutano au ibada kanisani. Hili halifai,” akasema Dkt Kidero.