ODONGO: Kalonzo, Mudavadi na Weta wajitafutie kura

Na CECIL ODONGO

KINARA wa ODM Raila Odinga amefanya vyema kutangaza kwamba hatamuunga au kuidhinisha mwanasiasa yeyote kuwania Urais wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Ingawa itatazamwa na mahasimu wake waliomuunga mkono miaka ya nyuma kama usaliti, kauli ya Bw Odinga inaafiki na itampa kila mwaniaji wa Urais nafasi ya kutia bidii kujitafutia kura.

Tayari waliokuwa viongozi wenzake katika muungano wa Nasa Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula Ford Kenya, walikuwa katika mstari wa mbele kumwaambia Bw Odinga asitishe azma yake ya Urais 2022 na ‘kurudisha’ mkono.

Japo ni kweli kwamba wanasiasa hawa walichangia kuvumisha urais wa Bw Odinga mnamo 2017, wengi wao hawajaonyesha juhudi zozote za kuimarisha umaarufu wao kote nchini kwa kuendesha kampeni kali.

Mabw Mudavadi na Wetang’ula wamekuwa wakikita kambi eneo la Magharibi kila wikendi wakizungumzia umoja wa jamii ya Waluhya kana kwamba kura za eneo hilo pekee ndizo zitawatunuku Urais.

Si siri kwamba lengo lao kuu ni kumzima kabisa umaarufu wa Bw Odinga katika siasa za eneo hilo lakini hata hiyo si rahisi kwa kuwa majemedari wa ODM pia wamekuwa wakiwarai wakazi kuwa viongozi hao wawili hawana ufuasi wowote kitaifa.

Japo uchaguzi bado u mbali, kukosa kujiuza katika maeneo mengine ya nchi na kuzamia siasa za Waluhya kunamswairi Bw Mudavadi kama anayesaka kuwa kigogo cha siasa za Magharibi huku akingoja kuidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Tangu Rais Kenyatta atangaze kwamba Kenya imeongozwa na makabila mawili na sasa ni wakati wa makabila mengine katika ibada ya mazishi ya mamake Bw Mudavadi mwezi uliopita, si siri viongozi wa eneo hilo walifasiri kauli hiyo kama ishara ya kumpigia debe makamu huyo wa Rais wa zamani.

Wakenya na wafuasi wa Nasa hawajawahi kusahau kwamba watatu hawa waliingia mitini wakati wa kuapishwa kwa kwa Bw Odinga mnamo Januari 30, 2018 kisha baadaye kuibuka na vijisababu ambavyo havina mashiko. Kwa hivyo, wao ndio wasaliti zaidi ikizingatiwa walikuwa wameahidi kuhudhuria hafla hiyo.

Bw Musyoka naye alinukuliwa akisema kuwa wafuasi wake watafikiria yeye ni mwendawazimu akimuunga Bw odinga kwa mara ya tatu ila anafaa afahamu kwamba hata kwake Ukambani umaarufu wake uko hatarini.

Magavana Kivutha Kibwana wa Makueni na Dkt Alfred Mutua wamekuwa wakimpinga Bw Musyoka na kumsawiri kama kiongozi ambaye hakusaidia eneo hilo kimaendeleo licha ya kuwa uongozini kwa zaidi ya miaka 30.

Kwa upande mwingine, muafaka katika Nasa unasema muda wa kuhudumu kwa muungano huo unafaa urefushwe kwa miaka mitano zaidi baada ya kukamilika kwa hatamu ya bunge la sasa.

Hata hivyo, ulisema tu Bw Odinga hafai kuwania Urais lakini haukutaja haswa anayefaa kuungwa mkono. Hata kama atajiondoa, itakuwa kibarua kikubwa kwa Mabw Mudavadi, Musyoka na Wetang’ula kuelewana kuhusu mpeperushaji bendera wa muungano.

Ni mapema sana kwa watatu hao kumshinikiza Bw Odinga awaunge mkono ilhali hata wao wenyewe hawana umoja wala hawajaonyesha ukakamavu wa kutwaa uongozi.

Habari zinazohusiana na hii