• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 5:36 PM
Tuchel awataka Chelsea kujihadhari dhidi ya mfumaji Luis Suarez wa Atletico Madrid

Tuchel awataka Chelsea kujihadhari dhidi ya mfumaji Luis Suarez wa Atletico Madrid

Na MASHIRIKA

CHELSEA watakosa huduma za beki Thiago Silva katika mchuano wa leo wa mkondo wa kwanza wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Atletico Madrid ya Uhispania.

Hata hivyo, viungo Kai Havertz na Christian Pulisic wamepona majeraha na kurejea kwao kunatarajiwa kupiga jeki kikosi hicho cha kocha Thomas Tuchel katika gozi litakalosakatiwa mjini Bucharest, Romania.

Kwa upande wao, Atletico wanaonolewa na kocha Diego Simeone watakosa maarifa ya Jose Gimenez, Sime Vrsaljko na Yannick Carrasco wanaouguza majeraha pamoja na Hector Herrera aliyepatikana na virusi vya corona.

Nafuu zaidi kwa miamba hao wa Uhispania ni kwamba washambuliaji wao Luis Suarez na Joao Felix kwa sasa wanajivunia fomu nzuri.

Beki Kieran Trippier pia hatakuwa sehemu ya kikosi cha Atletico kwa sababu amepigwa marufuku kwa kukiuka kanuni za mchezo wa kamari katika soka.

Chelsea watajitosa ugani wakijivunia rekodi ya kutoshindwa katika jumla ya mechi saba zilizopita chini ya kocha Thomas Tuchel aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Frank Lampard mnamo Januari 2021.

Japo kuhamishwa kwa mechi hiyo kutoka jijini Madrid hadi Bucharest ni nafuu zaidi kwa Chelsea, Tuchel amewataka masogora wake kujihadhari zaidi dhidi ya Suarez aliyewahi pia kuchezea Liverpool na Barcelona.

“Ni miongoni mwa wachezaji wanaojivunia tajriba pevu na uzoefu mkubwa kambini mwa Atletico. Bila shaka atatawaliwa na kiu ya kutuzamisha na ana uwezo huo iwapo hatadhibitiwa vyema,” akasema kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund na Paris Saint-Germain (PSG).

Suarez, 34, kwa sasa anaongoza orodha ya wafungaji bora kwenye kivumbi cha La Liga. Tuchel aliwahi kujaribu kumsajili fowadi huyo mwishoni mwa msimu uliopita ili atue kambini mwa PSG baada ya dalili zote kuashiria kwamba hakuwa anatakiwa tena na Barcelona.

Vikosi hivi vilipokutana kwa mara ya mwisho kwenye UEFA, Atletico walisajili ushindi wa 3-1 kwenye nusu-fainali za 2013-14.

Chini ya kocha Simeone, kikosi hicho kimetinga hatua za mwondoano za UEFA mara saba katika kipindi cha misimu minane iliyopita. Chelsea wanawinda fursa ya kufuzu kwa robo-fainali za UEFA kwa mara ya kwanza tangu wabanduliwe kwenye nusu-fainali za msimu wa 2013-14.

Hata hivyo, watakuwa na kibarua kigumu ikizingatiwa kwamba Simeone hajawahi kupoteza mechi ya mwondoano wa UEFA akidhibiti mikoba ya Atletico. Ameongoza waajiri wake kushinda mechi tisa na kuambulia sare mara nne.

Aidha, Atletico wamefungwa bao moja pekee katika mechi 12 zilizopita za hatua ya mwondoano wa UEFA. Goli hilo lilikuwa katika ushindi wa 2-1 waliosajili dhidi ya Real Madrid mnamo Mei 2017.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

WANGARI: Utaratibu wa Waislamu kuwazika waliofariki ni...

FKF: Bandari yaikaribisha Vihiga United