• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Kocha Flick ahimiza Bayern Munich watumie mechi ya leo ya UEFA dhidi ya Lazio kama jukwaa la kujinyanyua

Kocha Flick ahimiza Bayern Munich watumie mechi ya leo ya UEFA dhidi ya Lazio kama jukwaa la kujinyanyua

Na MASHIRIKA

KOCHA wa Bayern Munich Hansi Flick amewataka masogora wake kuitandika Lazio leo Jumanne kwenye mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) jijini Roma, Italia ili ushindi huo, iwapo wataupata, uwachochee kuanza tena kushinda michuano.

Chini ya Flick, Bayern wamenyakua jumla ya mataji sita katika kipindi cha miezi tisa iliyopita. Hata hivyo, wamepoteza alama nne muhimu katika mechi mbili zilizopita za Bundesliga baada ya kulazimishiwa sare ya 3-3 na Arminia kisha kupokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Eintracht Frankfurt.

Utepetevu huo umeshuhudiwa kambini mwa Bayern wiki chache baada ya miamba hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kupiga Tigres UANL ya Mexico 1-0 na kutwaa Kombe la Dunia nchini Qatar.

Hata hivyo, watashuka dimbani kumenyana na Lazio bila kujivunia maarifa ya kiungo Corentin Tolisso anayeuguza jeraha la goti na Thomas Muller anayeugua Covid-19.

“Hatutakuwa na sababu zozote za kutoshinda Lazio. Nina imani kwamba kikosi change kitatumia mchuano wa leo kujinyanyua na kujirejesha kwenye dira. Ni mechi spesheli ambayo tuna ulazima wa kushinda ili kuweka hai matumaini ya kutetea ufalme wa UEFA kwa mafanikio,” akasema Flick kwa kusisitiza kwamba anaridhishwa na motisha ya masogora wake.

Mechi kati ya Bayern na Lazio itakuwa ya kwanza kukutanisha vikosi hivyo viwili kwenye historia japo Lazio wanajivunia rekodi nzuri dhidi ya wapinzani kutoka Bundesliga. Kikosi hicho kimepoteza mechi moja pekee kati ya sita ambazo zimewahi kuwakutanisha na washiriki wa Bundesliga.

Lazio wametinga hatua ya 16-bora ya UEFA kwa mara ya kwanza baada ya miaka 21 licha ya kushinda mechi mbili pekee kati ya sita kwenye hatua ya makundi.

Kikosi hicho hata hivyo kinajivunia historia ya kufunga na kufungwa angalau bao moja katika kila mojawapo ya ya mechi zao 12 zilizopita kwenye UEFA.

Kwa upande wao, Bayern hawajawahi kushindwa kwenye michuano mitano iliyopita ya ugenini kwenye UEFA ambapo wameshinda mara tatu na kuambulia sare mara mbili.

Huu ni msimu wao wa 13 mfululizo kufuzu kwa hatua ya 16-bora kwenye soka ya UEFA. Ni Real Madrid (mara 24) na Barcelona (mara 17) ndio wanaowazidi. Kikosi hicho kimetinga hatua ya robo-fainali za UEFA mara 10 katika kipindi cha misimu 12 iliyopita.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

FKF: Bandari yaikaribisha Vihiga United

Chager afungua mwanya wa alama saba baada ya kushinda KCB...