• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
TAHARIRI: Vijana wasikubali kutumiwa kisiasa

TAHARIRI: Vijana wasikubali kutumiwa kisiasa

KITENGO CHA UHARIRI

MSIMU wa siasa umekuwa muda ambapo watu hukaidi kanuni zote za ustaarabu.

Wanasiasa, kwa kutumia hamasa za wananchi, hufanya mambo yanayoenda kinyume cha sheria na ambayo, yasipokabiliwa yanaweza kusababisha maafa kwa nchi.

Tayari baragumu la vita lipulizwa. Kila mwanasiasa ghafla ameanza kuona umuhimu wa vijana. Kuna wale wanaowashawishi kuwa vijana ni viongozi wa sasa, ilhali hawawezi kuwaruhusu wakaribie katika afisi zao. Vijana kwa kuwa rika lenye nguvu nyingi zisitotumika kwa manufaa yao binafsi wala taifa, wamelengwa kuwa vyombo vya uharibifu.

Unaposikiza semi za wanasiasa kuanzia leo hadi Agosti 9, 2022, hutakosa wakimtaja kijana. Wanawataja na kuwapa ahadi nyingi zisizotimizika, ili waingiwe na mori wa kutekeleza matakwa yao ya mchezo mchafu.

Wikendi mjini Kabarnet Kaunti ya Baringo, kulizuka makabiliano kati ya wafuasi wa Seneta Gideon Moi na Naibu Rais William Ruto. Wafuasi wa Bw Moi walifika kwenye mkutano ambao Dkt Ruto alikuwa akihutubia watu, wakaonyesha mabango yaliyoandika ‘Ruto Tosha’.

Nao wafuasi wa naibu Rais waliwarukia kwa mateke na mangumi huku wakishinikiza kuwa wawaue waliokwenda kuwachokoza.

Kwanza tunakemea kitendo cha wafuasi wa Bw Moi kwenda kuwachokoza wafuasi wa Dkt Ruto. Kuwatuma watu au watu kujipeleka kwenye mkutano usiowahusu na kubeba mabango ya kiongozi mwengine, ni uchokozi unaoweza kusababisha ghasia.

Lakini pia ni makosa kwa wafuasi wa Dkt Ruto kutaka kuwaua watu kwa madai ya kuzua fujo. Sheria za Kenya ziko wazi kuhusu uhalifu. Kama wafuasi hao walihisi kuwa wenzao walikuwa wanavunja sheria yoyote, kulikuwa na maafisa wa usalama wa kutosha. Wangewasilisha malalamishi kwao na bila shaka wangechukua hatua.

Mtindo huu wa wanasiasa kudhamini wahuni na magenge sasa umesambaa katika kaunti nyingi, ikiwemo ya Homa Bay. Wanasiasa wawili wamelia kuwa wenzao wanawalipa na kuwahami vijana iili wavuruge mikutano yao.

Wanasiasa wanawahadaa raia wapigane na kuuana kwa ajili yao, kisha jioni wanasiasa hao mahasimu waketi pamoja wakijiburudisha na kucheka jinsi kila mmoja wao alivyo na uwezo wa kuvutia watu upande wake.

Kabla mtu hajachukua hatua kushambulia mwenzake kwa sababu ya kampeni, ajiulize kama mwanasiasa huyo atasimama naye atakapoumizwa au kutiwa mikononi mwa polisi.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Jinsi mihadarati inavyoua vijana kwa maradhi...

Osoro asimulia mahangaiko aliyopitia mikononi mwa polisi...