• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 3:23 PM
Osoro asimulia mahangaiko aliyopitia mikononi mwa polisi alipozuiwa kuhudhuria mazishi ya Nyachae

Osoro asimulia mahangaiko aliyopitia mikononi mwa polisi alipozuiwa kuhudhuria mazishi ya Nyachae

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Mugirango Kusini, Bw Silvanus Osoro amedai mahangaiko aliyopitishwa wakati wa maziko ya Mzee Simeon Nyachae yana mkono wa chochezi za kisiasa.

Bw Osoro pamoja na Naibu Gavana wa Kisii, Bw Joash Maangi walizuiwa kuhudhuria hafla ya mazishi ya Waziri huyo wa zamani, kwa tuhuma za kuwa na mipango kuyavuruga.

Mzee Nyachae alizikwa nyumbani katika kijiji cha Nyosia, Kaunti ya Kisii mnamo Februari 15, 2021.

Mabw Osoro na Maangi walitiwa nguvuni na maafisa wa polisi, ambapo walisalia kuzuizini kwa zaidi ya saa 12 katika Kituo cha Polisi cha Keroka.

Kulingana na Osoro, alizungushwa eneo la Nyanza, katika kile amedai “kuna kiongozi fulani anayejaribu kuonyesha ubabe wa mamlaka”, kwa sababu ya msimamo wake kuwa mwandani na mtetezi wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto.

Kwenye kurasa zake za mitandao, mbunge huyo amechapisha akieleza kwamba hatua ya kuzuiwa kuhudhuria hafla ya kumpa heshima za mwisho Mzee Nyachae, ilichochewa kisiasa, kutokana na tofauti zinazoendelea kujiri kati ya kundi la Tangatanga (linaloegemea upande wa Dkt Ruto) na Kieleweke (linaloegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Bw Raila Odinga).

“Charles Nyachae (mwanawe Mzee Nyachae) na mimi ni marafiki wa karibu. Hutangamana naye nikiwa Nairobi. Yeye ni kama kaka yangu mkubwa. Nilimshawishi ajiunge na vuguvugu la ‘Hastla’, na kuunga mkono Dkt Ruto, na akakubali…Tangu afiwe na babake nimekuwa naye katika makazi yake Nairobi, kila siku,” Bw Osoro akasimulia kwenye Facebook.

Kwa mujibu wa maelezo ya mbunge huyo, siku ambayo hakumtembelea Bw Charles, ni aliyoratibu Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kukutana na marafiki na waandalizi wa mazishi ya mwendazake, kwa kile anahoji ulikuwa uamuzi wa hiari.

Hata hivyo, anasema alikutana na Bw Charles siku iliyofuata.

“Siku ya mazishi, nikijiandaa kukaa niliondolewa na Kamanda wa Kaunti na CCIO (afisa kutoka kitengo cha uhalifu na jinai – DCI), walioniambia wana kila sababu kuamini nilikuwa na mipango viongozi fulani wazomewe. Walinishurutisha niandamane nao, sikukataa,” Osoro akaelezea.

Mbunge huyo alisimulia, ilikuwa ziara ya kutoka kituo kimoja cha polisi hadi kingine, chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi.

“Ulikuwa msafara wa karibu magari manane (nilihisi vyema), yakiendeshwa kwa kasi ya kilomita 180 kila saa, huku nikizingirwa na maafisa watatu wakuu waliojihami,” akafafanua.

“Nilizungushwa eneo la Nyanza, kilele kikawa kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Keroka, nikaandikiwa mashtaka ya uchochezi na kujaribu kuzua fujo,” akasema akionekana kusuta kiongozi aliyedai anajaribu kuonyesha ubabe wa mamlaka japo hakumtaja.

Mbunge huyo alisema maafisa waliotumiwa walimlazimisha awape nambari zake za siri za kufungua simu, ila alikataa akihoji hatua hiyo “ni hujuma na iliyokiuka haki zake”.

Anaeleza aliwafungulia, kwa uwepo wake, na baada ya kuipekua hawakupata walichotafuta.

“Walinieleza ‘mheshimiwa usijali, siasa huwa hivyo. Tunahisi vibaya, ila tuko kazi. Tukipata mashtaka, tutakwambia,” Osoro akadokeza, akisema alisalia kizuizini kati ya saa nne asubuhi hadi saa saba usiku.

Alifichua kwamba aliachiliwa bila kufunguliwa mashtaka yoyote, na alipotaka majibu kwa nini ahangaishwe alielezwa “raia walikita kambi kituoni wakitaka aachiliwe huru, maafisa wa usalama wakijaribu kuepuka malumbano”.

Akikashifu kiongozi aliyebana majina yake, kwenye chapisho hilo la Facebook, Bw Osoro alisisitiza hatabadilisha msimamo wake.

Mbunge huyo akishikilia anahangaishwa kwa sababu ya uamuzi wake kuunga mkono azma ya Naibu wa Rais Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022, alisema taarifa ya majasusi ilidai alikuwa amelipa wahuni wawashambulie kwa maneno baadhi ya viongozi wakizungumza katika hafla ya mazishi ya Mzee Nyachae.

“Ikiwa nililipa wahuni, kwa nini nikatiwa nguvuni peke yangu? Kwa nini wanaodaiwa nilitaka kuwatumia hawakukamatwa?” Osoro akataka kujua.

Februari 1, 2021, katika mazishi ya babake Naibu Gavana wa Kisii, Bw Joash Maangi, Mzee Abel Gongera, Osoro na mbunge wa Dagoretti Simba Arati waliangushiana makonde, mbele ya Dkt Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Vijana wasikubali kutumiwa kisiasa

Mswada wa BBI wakaribia kuingia katika Bunge la Kitaifa