Mswada wa BBI wakaribia kuingia katika Bunge la Kitaifa

Na SAMMY WAWERU

KAUNTI ya Murang’a imejiunga na orodha ya kaunti ambazo zimepitisha Mswada wa Ripoti ya Mpango wa Maridhiano, BBI.

Hii ni baada ya madiwani wa kaunti hiyo mnamo Jumanne kuandaa kikao kujadili kuhusu mswada huo unaopendekeza Katiba kufanyiwa marekebisho na kuupitisha.

Kwenye kikao hicho, MCA wote waliohudhuria walipitisha BBI.

“Hakujakuwa na waliosusia kupiga kura wala waliopinga, mswada huu umepitishwa kwa kura 53 Murang’a,” akatangaza spika wa bunge la kaunti hiyo.

Kaunti zingine eneo la Kati ambazo zimepitisha BBI ni pamoja na Laikipia na Nyeri.

Zaidi ya kaunti 25 zimeidhinisha ripoti hiyo, nah ii ikiwa na maana kuwa sasa itaelekezwa bunge la kitaifa kujadiliwa ili kura ya maamuzi kuandaliwa baadaye mwaka huu wa 2021.

BBI ilihitaji kaunti zisizopungua 24 kuidhinishwa ili kuelekezwa bunge la kitaifa kwa minajili ya refaranda.

Kaunti mbalimbali nchini zinaendelea kujadili mswada huo, ili kuupitisha au kuuangusha.

BBI ilizinduliwa kufuatia salamu za maridhiano maarufu kama Hnadisheki, kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, ambapo waliahidiana kuunganisha taifa.

Naibu wa Rais, Dkt William Ruto amekuwa akikosoa BBI, akihoji Handisheki inalenga kutatiza safari yake kuingia Ikulu 2022.

Eneo la Mlima limetajwa kuwa ngome ya Dkt Ruto, ila kupitishwa kwa BBI Murang’a, Nyeri na Laikipia inaashiria piga kisiasa kwa Naibu Rais.

Kuna kesi saba ambazo kwa pamoja zinapinga BBI. Hatima ya mswada huo hivyo iko mikononi mwa mahakama.

Habari zinazohusiana na hii