Masoud Juma, Duncao Ochieng’ wachana nyavu katika wikendi nzuri kwa Wakenya ughaibuni

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA wanaosakata kabumbu nje ya nchi walikuwa na siku nzuri viwanjani wikendi wakiongozwa na Masud Juma na Duncan Otieno waliofungia klabu zao bao la ushindi.

Haya hapa matokeo ya jinsi mambo yalivyokuwa uwanjani kwa Wakenya ughaibuni:

Morocco

Sajili mpya wa Difaa Hassani El Jadidi (DHJ) Masud Juma alifunga bao lake la kwanza kabisa na lingine likakataliwa katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Rapide Oued Zem kwenye Ligi Kuu ya Botola Pro Inwi mnamo Jumapili.

Beki Khalid El Ghafouli alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 16 kabla ya Juma, ambaye msimu uliopita alikuwa JS Kabylie nchini Algeria, kufunga la ushindi dakika ya 36. Wote walisukuma makombora makali yaliyojaa wavuni. Juma alipata bao lake la pili dakika ya 82, lakini likakataliwa na teknolojia ya VAR. Ushindi huo wa pili mfululizo umesaidia DHJ kuruka juu kutoka nafasi ya pili kutoka mwisho hadi nambari 10. Imezoa alama nane kutokana na michuano saba. Mchuano huo ulikuwa wa pili kwa mshambuliaji huyo ambaye timu yake ilizamisha wageni Nahdat Zemamra 1-0 katika mechi yake ya kwanza Februari 13. Itamenyana na miamba Raja Casablanca wanaoshikilia nafasi ya pili, katika mechi ijayo hapo Februari 28.

Uingereza

Beki Clarke Oduor alikuwa kitini klabu yake ya Barnsley ikiendelea kutetemesha kwenye Ligi ya Daraja ya Pili ilipochabanga wenyeji Bristol City 1-0 Jumamosi. Muingereza Carlton Morris alifunga bao la ushindi katika kipindi cha pili. Ushindi huo ni wa tatu mfululizo kwa Barnsley ambayo inaweza kuanza kuota kupigania tiketi ya Ligi Kuu tofauti na msimu uliopita ilipohitaji bao kutoka kwa Oduor katika mechi ya mwisho kuponea kuangukiwa na shoka. Barnsley inafunga mduara wa 10-bora kwa alama 45 kutokana na mechi 30. Iko alama nne nje ya mduara wa sita-bora ambao nambari tatu hadi sita huwania tiketi moja inayosalia ya kupandishwa daraja. Barnsley itaalika Stoke katika mechi yake ijayo mnamo Februari 24.

Tanzania

Biashara Mara United ilijinyanyua kutoka kwa kichapo cha goli 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi Simba SC kwa kupepeta Ruvu Shooting 3-0 uwanjani Karume kwenye Ligi Kuu Bara hapo Jumapili. Vijana hao wa kocha Francis Baraza walizoa alama tatu kupitia mabao ya Christian Zigah, Lenny Kisu na Yusuph Athuman. Biashara inakamata nafasi ya nne kwenye ligi hiyo ya klabu 18 baada ya kuzoa alama 35 kutokana na michuano 21. Young Africans, ambayo imeajiri kipa Mkenya Farouk Shikalo, inaongoza jedwali kwa alama 49. Ililemea Mtibwa Sugar 1-0 Jumamosi. Simba, ambayo inashikilia nafasi ya pili kwa alama 42 kutokana na michuano 18, itaalika mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Al Ahly kutoka Misri jijini Dar es Salama hapo Februari 23. Beki Joash ‘Berlin Wall’ Onyango na kiungo Francis Kahata wanachezea Simba. Walikuwa katika kikosi kilichokung’uta AS Vita nchini DR Congo katika mechi yao ya kwanza ya Kundi A mnamo Februari 12. Vita itakabana koo na Al Merrikh katika mchuano mwingine wa kundi hilo Jumanne.

Ethiopia

Saint George anayochezea kipa Patrick Matasi ilikanyaga Adama City 4-2 uwanjani Bahir Dar kwenye Ligi Kuu na kumaliza msururu wa sare tatu Jumamosi. Timu ya Saint George, ambayo imepaa nafasi tatu hadi nambari tatu kwa alama 21 kutokana na michuano 11, ilitinga magoli kupitia Abel Endale, Getaneh Kebede na Amanuel Gebremichael aliyefunga mawili. Fisseha Thomas Tsegaye Balcha walifungia Adama.

Zambia

Kiungo mkabaji Duncan Otieno alifungia Lusaka Dynamos bao la pekee na la ushindi dhidi ya Buildcon dakika ya mwisho kwenye Ligi Kuu mnamo Jumapili. Lusaka, ambayo imezoa alama 10 katika michuano minne iliyopita, inashikilia nafasi ya tatu kwa alama 30 baada ya kujibwaga uwanjani mara 18. Zanaco inaongoza kwa alama 32 kutokana na mechi 18 nayo Zesco, ambayo imeajiri Wakenya Ian Otieno, Jesse Were na John Makwata, inapatikana katika nafasi ya pili alama moja nyuma na pia imesakata mechi moja chache. Kiungo mshambuliaji Duke Abuya alikuwa katika kikosi cha Nkana kilichopoteza 2-1 Jumapili dhidi ya TAS Casablanca nchini Morocco kwenye mechi ya kuingia makundi ya Kombe la Mashirikisho Afrika, lakini kikasonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2. Mabeki Mahmoud Bentayg na Ayman Dairani walipachika mabao ya TAS katika kipindi cha kwanza naye Simon Mulenga akatikisa nyavu za wenyeji hao wao. Nkana ilikamilisha mchuano huo watu 10 baada ya beki Mghana Richard Ocran kuonyeshwa kadi nyekundu.

Nao beki David Owino ‘Calabar’ na kipa Shaaban Odhoji walikuwa katika kikosi cha NAPSA Stars ambacho kilibandua waajiri wao wa zamani Gor Mahia kwenye Kombe la Mashirikisho la Africa kwa jumla ya mabao 3-2 Jumapili.

Samuel Onyango na Clifton Miheso walisukuma wavuni mabao ya Gor ambayo ilikuwa mbioni kujikatia tiketi ya kuingia makundi kabla ya penalti kutoka kwa Emanuel Mayuka dakika ya mwisho kuzima matumaini hayo.

Kuna madai kuwa timu ya Gor ilikerwa na kazi ya refa kuadhibu Gor kwa kuwapa NAPSA penalti. Tetesi hizo zinasema kuwa Gor walishambulia refa huyo pamoja na kusababisha uharibu uwanjani. Miamba hao wa Kenya sasa wako katika hatari ya kupigwa faini ama marufuku ama kupokea adhabu hizo zote kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Austine Banda alifungia NAPSA goli la kwanza katika kipindi cha kwanza.

Uhispania

Las Palmas anayochezea beki Ismael Athumani Gonzalez ilipepeta wageni wao Cartagena 2-0 kupitia mabao ya Crespo Garcia na Maikel (penalti) kwenye Ligi ya Daraja ya Pili, Jumamosi. Gonzalez hakutumiwa katika mchuano huo. Las Palmas wako katika nafasi ya 10 kwenye ligi hiyo kwa alama 35 kutokana na michuano 26. Cartagena ni nambari 19 kwenye ligi hiyo ya timu 22 ambayo nne za mwisho zitashushwa ngazi. Las Palmas itazuru nambari 22 Castellon katika mechi ijayo hapo Februari 27.

Ugiriki

Ionikos anayochezea beki Abud Omar ilitupa uongozi ikitoka 1-1 dhidi ya Levadiakos katika mechi ya Ligi ya Daraja ya Pili kati ya nambari mbili na tatu, mtawalia. Ergotelis iko kileleni kwa alama 19 kutokana na michuano tisa. Ionikos na Levadiakos zimesakata mechi 10. Zimeambulia alama 18 na 17, mtawalia. Mechi ya Ionikos ijayo ni dhidi ya nambari nane PAE Chania hapo Februari 27.

Afrika Kusini

Kaizer Chiefs inayoajiri kiungo Anthony ‘Teddy’ Akumu iligawana alama na Supersport United katika sare ya 1-1 kwenye Ligi Kuu, Jumamosi. Akumu, ambaye alikosa mechi iliyopita dhidi ya AmaZulu (Februari 17), alichezeshwa dakika 90. Chiefs itakuwa na kibarua cha Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Horoya kutoka Guinea hapo Februari 23. Horoya inaongoza Kundi C kwa alama tatu baada ya kuchabanga Petro Atletico 2-0 Februari 13. Chiefs haikusafiri nchini Morocco kukabiliana na Wydad Casablanca baada ya taifa hilo kuwanyima vibali vya kusafiria kwa hofu ya maambukizi ya virusi vya corona. Mechi ya Kundi B kati ya viongozi Mamelodi Sundowns na nambari tatu CR Belouizdad hapo Februari 23 nchini Algeria ilifutiliwa mbali baada ya Algeria kuweka masharti makali ya kiafya kwa wasafiri.

Serbia

Kiungo Mkenya Richard Odada bado anaendelea kusubiri kujumuishwa katika kikosi cha siku ya mechi cha Red Star Belgrade ambayo ilidumisha rekodi ya kutoshindwa kwa kuzaba wenyeji Sp. Subotica 2-1 kwenye Ligi Kuu ya Serbia, Jumapili. Odada alijiunga na timu hiyo katika kipindi kifupi cha uhamisho cha Januari. Red Star inaongoza ligi hiyo kwa alama 62 kutokana na ushindi 20 na sare mbili. Timu hiyo itakabiliana na AC Milan katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Uropa ya raundi ya 32-bora uwanjani San Siro. Red Star ilikabwa 2-2 nyumbani mnamo Februari 18.