• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Difenda David Alaba kuondoka Bayern Munich baada ya kuwahudumia kwa miaka 13

Difenda David Alaba kuondoka Bayern Munich baada ya kuwahudumia kwa miaka 13

Na MASHIRIKA

BEKI matata raia wa Austria, David Alaba amethibitisha kwamba ataondoka rasmi kambini mwa Bayern Munich mwishoni mwa msimu huu baada ya kukosa kuafikiana kuhusu mkataba mpya.

Nyota huyo aliingia katika sajili ya Bayern mnamo 2008 na amekuwa katika mazungumzo na miamba hao wa soka ya Ujerumani na bara Ulaya kuhusu uwezekano wa kurefusha kandarasi yake inayotamatika mwishoni mwa msimu huu.

Alaba, 28, amefunga jumla ya mabao 33 kutokana na mechi 417 akivalia jezi za Bayern na alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshindia mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mataji ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2013 na 2020.

“Hayakuwa maamuzi rahisi kwa sababu nimekuwa nikichezea Bayern kwa miaka 13 na kikosi hiki kimeishia kuwa sehemu ya maisha yangu,” akasema Alaba anayehusishwa na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona au Real Madrid japo anahemewa pia na vikosi kadhaa vya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Manchester United, Liverpool, Manchester City, Atletico Madrid na Paris Saint-Germain (PSG) ni miongoni mwa klabu nyinginezo za bara Ulaya zinazohemea maarifa ya Alaba.

Mwanasoka huyo kwa sasa ndiye mchezaji wa sita ghali zaidi kambini mwa Bayern baada ya Robert Lewandowski, Manuel Neuer, Thomas Muller, Lucas Hernandez na Jerome Boateng.

Tangu awajibishwe na Bayern kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17 mnamo Februari 2010, Alaba amewaongoza miamba hao kutia kapuni mataji tisa ya Bundesliga na sita ya German Cup.

Alikuwa pia sehemu ya kikosi cha Bayern kilichotia kibindoni Kombe la Dunia wiki mbili zilizopita baada ya waajiri wake kupepeta Tigres UANL ya Mexico 1-0 nchini Qatar.

Ushindi huo uliwezesha Bayern kutia kibindoni taji lao la sita chini ya kipindi cha miezi tisa iliyopita. Bayern wanaonolewa na kocha Hansi Flick, wametawazwa mabingwa wa Uefa Super Cup, German Super Cup na kwa sasa ndio wafalme wa dunia, ufanisi ambao umewashuhudia wakitwaa jumla ya mataji matatu kwa mpigo baada ya kunyanyua makombe mengine matatu katika kampeni za msimu uliopita wa 2019-20.

Alaba ametawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka nchini Austria mara saba na alitwaa tuzo hiyo mara sita mfululizo kati ya 2011 na 2016.

Tangu avalie jezi ya timu ya taifa ya Austria kwa mara ya kwanza mnamo 2009 akiwa na umri wa miaka 17 pekee, Alaba amechezea kikosi hicho katika zaidi ya mechi 70 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Austria kwenye fainali za Euro 2016 nchini Ufaransa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Jepchirchir aongezwa kwenye orodha wa wawakilishi wa Kenya...

Chipukizi Mason Greenwood sasa kuchezea Manchester United...