Atupwa jela miaka mitatu kwa kuiba chupi

Na SAMMY WAWERU

MWANAUME mmmoja amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuiba chupi.

Bw Stephen Ochieng alipokezwa adhabu hiyo na mahakama ya Makadara, kufuatia kesi iliyowasilishwa ambapo alipatikana makosa ya kuiba chupi katika makao makuu ya Shirika la Huduma kwa Taifa (NYS), jijini Nairobi.

Kulingana na uamuzi uliotolewa na hakimu mkuu, Bw Heston Nyaga, mshtakiwa aliingia katika nyumba ya Antony Munene na kuiba chupi, spika ya redio na nyundo ndogo.

Mlalamishi alikuwa amelala wakati wa tukio hilo.

Korti ilielezwa kwamba walinzi wa jengo analoishi Bw Munene walitazama mshtakiwa akijaribu kutoroka, ndiposa akatiwa nguvuni.

Ochieng pia alipatikana na makosa mengine ya kutekeleza wizi katika jengo hilo mwaka wa 2016.

“Tabia yake inawiana na ya mwingine aliyekuwa akihangaisha wakazi wa Kilimani, Nairobi, ila huyu ni mhalifu wa eneo la NYS,” Hakimu Nyaga akasema wakati akitoa uamuzi.