Marcelo Bielsa wa Leeds United kufanya maamuzi kuhusu mustakabali wake wa ukocha ugani Elland Road kabla ya msimu huu wa EPL kukamilika

Na MASHIRIKA

KOCHA Marcelo Bielsa amesema atakuwa radhi kutia saini mkataba mpya kambini mwa Leeds United ila angependa aachiwe fursa ya kufanya maamuzi kuhusu mustakali wake wa ukufunzi mwishoni mwa kampeni za msimu huu wa 2020-21.

Kandarasi ya sasa kati ya Bielsa na Leeds United ugani Elland Road inatarajiwa kutamatika mwishoni mwa muhula huu na mmiliki wa kikosi hicho, Andrea Radrizzani, amesisitiza kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake ni kumshuhudia Bielsa akisalia kudhibiti mikoba yao.

“Iwapo waajiri wangu watataka jibu kuhusu maamuzi mustakabali wangu wa ukufunzi kabla ya mwisho wa msimu huu, basi nitakuwa radhi kufanya hivyo. Hata hivyo, ingekuwa vyema iwapo wataniachia kufichua mipango yangu mwisho wa muhula,” akasema Bielsa aliyewaongoza Leeds United kurejea katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuwa nje kwa miaka 16.

Bielsa, 65, aliteuliwa kudhibiti mikoba ya Leeds United mnamo Juni 2018 na akaongoza kikosi hicho kutwaa taji la Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) mnamo 2019-20.

Kufikia sasa, kikosi cha Bielsa ambaye ni raia wa Argentina, kinashikilia nafasi ya 12 kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 32 sawa na Crystal Palace.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO