‘Wakristo 800 waliuawa eneo la Sanduku la Agano’

MARY WANGARI na MASHIRIKA

WATU 800 waliripotiwa kuuawa katika mauaji ya halaiki kwenye kanisa moja la Kikristo mjini Axum, Uhabeshi, ambapo waumini wanaamini Sanduku la Agano limehifadhiwa.

Kanisa hilo la St Mary of Zion lilikuwa eneo la hifadhi kwa wakimbizi wa Uhabeshi katika eneo la Tigray wanaotoroka mapigano ya kikabila nchini humo.

Masaibu yalikumba kanisa hilo katikati mwa mwaka 2020 wakati wa mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi waliojihami ambapo mamia ya watu walifariki jambo ambalo limegunduliwa sasa.

Idadi inayokadiriwa ya vifo ilitofautiana kutokana na hatua ya kukata laini za simu na kuwapiga marufuku wanahabari eneo la Tigray.

Huku eneo hilo likianza kutangamana na ulimwengu wa nje, mzee wa kanisa hilo aliyechelea kutajwa kwa kuwa ni mkazi wa Axum, alisema watu 800 waliuawa.

“Tukienda katika maeneo ya vijijini, hali ni mbaya zaidi,” alisema akisimulia yaliyotendeka Novemba 2020.

Waziri Mkuu Uhabeshi, Abiy Ahmed, aliyeshinda Tuzo ya Amani ya Nobeli 2019 kwa kuwezesha amani na taifa jirani la Eritrea, alitangaza mapigano hayo wakati ulimwengu ulikuwa umeangazia chaguzi za Amerika.

Alishutumu vikosi kutoka eneo la Tigray, ambavyo viongozi wake walitawala Uhabeshi kwa takriban miongo mitatu kabla yeye kuchukua usukani, dhidi ya kushambulia jeshi la Uhabeshi.

Viongozi wa Tigray walitaja hatua hiyo kama ya kujikinga baada ya miezi kadhaa ya taharuki.

Huku ulimwengu uking’ang’ana kupenya Tigray kuchunguza maovu yanayoshukiwa kutekelezwa na pande zote mbili na kupeleka msaada kwa mamilioni ya watu wanaokabiliwa na njaa, waziri mkuu huyo amekataa “kuingiliwa” na mataifa ya nje.

Alitangaza ushindi mwishoni mwa Novemba na kusema hakuna raia aliyeuawa.

Serikali yake imekana kuwepo kwa maelfu ya wanajeshi kutoka Eritrea, ambao ni adui wa muda mrefu wa viongozi wa Tigray.

Mauaji hayo yangali yanaendelea kulingana na mhubiri huyo akisema alisaidia kuwazika watu watatu wiki iliyotangulia.