Everton kujenga uwanja mpya wa kubeba mashabiki 52,000 kwa Sh71 bilioni

Na MASHIRIKA

MIPANGO ya Everton kujenga uwanja mpya wenye uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 52,000 walioketi imeidhinishwa bila pingamizi na wakuu wote wa Manispaa ya jiji la Merseyside, Uingereza.

Uwanja huo utakaojengwa katika eneo la Bramley-Moore Dock utaanza kutumiwa rasmi kuandalia mechi mnamo 2024.

Ujenzi wa uwanja huo unatarajiwa kugharimu kima cha Sh71 bilioni na utabuni nafasi 15,000 za ajira baada ya kukamilika.

Mipango mingine ya Everton ya kuukarabati uwanja wao wa sasa wa nyumbani wa Goodison Park kwa kima cha Sh11 bilioni pia imeidhinishwa na wadau wa Merseyside.

Kufikia sasa, Everton wanaonolewa na kocha Carlo Ancelotti wametandaza jumla ya mechi 24 ambapo wameshinda 12, kuambulia sare mara nne kupoteza nane katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Matokeo hayo yanawaweka katika nafasi ya saba kwa alama 40 sawa na watani wao wakuu jijini Merseyside, Liverpool, ambao ni mabingwa watetezi wa taji la EPL.

Everton wamekuwa wakichezea mechi zao za nyumbani ugani Goodison Park tangu 1892 na mipango ya kujenga uga mpya ilianzishwa miaka 25 iliyopita.

Baada ya kujengwa kwa uwanja mpya, Everton wamethibitisha kwamba watatumia Sh7.7 bilioni zaidi kujenga kituo kitakachokuwa hifadhi ya turathi za kikosi chao katika eneo la Hydraulic Tower karibu na uwanja wa Goodison Park.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO