• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Simba SC inayoajiri Wakenya Joash Onyango na Francis Kahata yarurua Al Ahly dimba la Klabu Bingwa Afrika

Simba SC inayoajiri Wakenya Joash Onyango na Francis Kahata yarurua Al Ahly dimba la Klabu Bingwa Afrika

Na GEOFFREY ANENE

MIAMBA wa soka nchini Tanzania, Simba SC wamechupa uongozini mwa Kundi A kwenye Klabu Bingwa Afrika baada ya kuduwaza washikilizi wa taji hilo Al Ahly 1-0 katika mechi ya kusisimua jijini Dar es Salaam, Jumanne.

Simba, ambao wameajiri Wakenya Joash “Berlin Wall” Onyango na Francis Kahata, walizamisha Mafirauni hao kupitia bao la Luis Miquissone.

Kiungo huyo kutoka Msumbiji alimwaga kipa Mohamed El Shenawy (nahodha) dakika ya 31. Kila mmoja alikuwa ameshambulia ngome ya mwenzake vilivyo kabla ya Miquissone kupatia Simba bao hilo muhimu.

Kocha Seleman Matola alifanya mabadiliko manne katika kipindi cha pili ikiwemo kuingiza Kahata katika nafasi ya Miquissone dakika ya 87.

Al Ahly ya kocha Pitso Mosimane ilifanya mabadiliko yote matano katika kipindi cha pili, lakini juhudi zake za kuvunja ngome ya Simba hazikufua dafu.

Simba, ambayo ilikung’uta AS Vita 1-0 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mechi yake ya ufunguzi mnamo Februari 12, inaongoza kwa alama sita.

Imeng’oa kileleni Al Ahly ambayo ilichabanga Al Merrikh kutoka Sudan 3-0 nchini Misri mnamo Februari 16.

Vita ni ya pili kwa alama tatu baada ya kupepeta Al Merrikh 4-1 Jumanne.

Wenyeji Al Merrikh walitangulia kuona lango la Vita kupitia kwa beki Elsamani Saadeldin dakika ya nane. Obed Mukokiani alifungia Vita mabao mawili nao Djuma Shabani na Amede Masasi wakachangia goli moja kila mmoja.

Al Merrikh haina alama baada ya michuano ya raundi mbili za kwanza za kundi hilo. Simba itazuru Al Merrikh hapo Machi 5 siku mbayo Al Ahly itaalika Vita jijini Cairo. Timu zitakazokamilisha mechi za makundi katika nafasi mbili za kwanza zitaingia robo-fainali. Simba imewahi kufika robo-fainali mara moja ilipobanduliwa na TP Mazembe kutoka DR Congo kwa jumla ya mabao 4-1 msimu 2018-2019. Baada ya kupiga Vita na Al Ahly, imeanza kujiweka pazuri kufuzu kwa mara ya pili.

  • Tags

You can share this post!

Everton kujenga uwanja mpya wa kubeba mashabiki 52,000 kwa...

Olunga hatimaye achezeshwa mechi nzima na Al Duhail ikizima...