• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Olunga hatimaye achezeshwa mechi nzima na Al Duhail ikizima Al Gharafa ligini

Olunga hatimaye achezeshwa mechi nzima na Al Duhail ikizima Al Gharafa ligini

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Michael Olunga alichezeshwa mechi nzima kwa mara ya kwanza na waajiri wake wapya Al Duhail wakishinda wenyeji Al Gharafa 2-1 kwenye Ligi Kuu ya Qatar mnamo Jumatatu usiku.

Engineer anavyofahamika Olunga kwa jina la utani, amechezea mabingwa hao wa Qatar michuano minane tangu awasili kutoka Kashiwa Reysol mnamo Januari 12.

Kabla ya Februari 22, mshambuliaji huyo Mkenya alikuwa ameonja dakika 66 dhidi ya viongozi wa Ligi Kuu ya Qatar (Januari 12), 45 wakivaana na Qatar SC (Januari 19) na 70 dhidi ya Al Ahli Doha (Januari 25).

Pia, alisakata dakika 45 dhidi ya mabingwa wa Afrika na Misri Al Ahly (Februari 4), 60 alikutana na wafalme wa Klabu Bingwa Asia Ulsan Hyundai (Februari 7), 31 dhidi ya Al Rayyan (Februari 14) na 59 wakigaragazana na Al Gharafa (Februari 18).

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Kenya amefungia waajiri wake wapya mabao manne. Alipachika magoli matatu katika mechi ya Kombe la Amir ambayo Al Duhail ilibwaga Al Ahli Doha 6-0 na kuingia robo-fainali na moja dhidi ya Al Rayyan ligini. Hajaona lango katika michuano sita ikiwemo miwili iliyopita. Sababu kuu ya mabao kupiga chenga Olunga haijabanika wazi, ingawa huenda ni ushindani mkubwa ya kila mchezaji kambini Al Duhail kutaka kufunga. Pia, Olunga hajazoea ligi ya Qatar. Huenda pia uchovu umemwingia.

Msimu wa 2020 wa Japan ulikatika Januari 4, huku Olunga akiwa amechezea Kashiwa michuano 35 katika mashindano yote na kuibuka mfungaji bora kwa mabao 28 ligini. Al Duhail itaalika mabingwa watetezi wa dimba la Qatar Cup, Al Sadd hapo Februari 26.

Ni mechi yenye umuhimu mkubwa ambayo Olunga atatumai kushinda taji lake la kwanza katika klabu ya kigeni tangu asaidie Kashiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Daraja ya Pili Japan mwaka 2019.

You can share this post!

Simba SC inayoajiri Wakenya Joash Onyango na Francis Kahata...

Kifo cha Mbunge chaongeza mkosi kwa Bunge la 12