Kwani kuliendaje?

Na CHARLES WASONGA

KUPITISHWA kwa Mswada wa BBI katika kaunti ambazo ni ngome ya Naibu Rais William Ruto kumewaacha wengi na maswali mengi kuwa kuwa ilitarajiwa madiwani wa kaunti hizo wangeuangusha.

Mabunge ya kaunti za Bomet, Narok, Muranga na Nakuru ambako Dkt Ruto ana ushawishi mkubwa ni miongoni mwa zaidi ya mabunge 24 zaidi yaliyopitisha mswada huo Jumanne.

Hayo yametokea kama mshtuko kwa Dkt Ruto ambaye amekuwa akipinga mswada huo wa BBI akidai unalenga kubuni nyadhifa zaidi kwa matajiri viongozi na kupuuza masilahi ya walalahoi.

Kaunti zingine zilizopitisha mswada huo Jumanne ni; Bungoma, Kitui, Lamu, Garissa, Kirinyaga, Nyeri, Machakos, Taita Taveta, Nyamira, Nyandarua na Makueni. Zingine zilikuwa; Migori, Mombasa, Kwale, Kakamega, Isiolo na Kiambu.

Kupitishwa kwa mswada huo katika kaunti hizo sasa kumefikisha 38 idadi ya kaunti ambazo zimeudhinisha na kutoa nafasi kwa kura ya maamuzi.

Kufikia Jumatatu, ni mabunge 12 yalikuwa yameupitisha mswada huo huku bunge la kaunti ya Baringo likiwa la kipekee ambalo liliuangusha wiki jana.

Katika kaunti ya Murang’a, madiwani walimkashifu seneta wao Irungu Kang’ata ambaye alimwandikia Rais Uhuru Kenyatta barua akidai BBI maarufu huko na eneo zima la Mlima Kenya.

Madiwani hao walitoa kauli za “Kang’ata Must Go!” (Kang’ata Sharti Aende) punde baada ya kujadili na kuupitisha mswada huo katika kikao kilichohudhuriwa na Gavana Mwangi Wa Iria. Madiwani wote 53 walihudhuria kikao cha Jumanne na kupiga kura ya NDIO.

Kwenye barua hiyo ambayo Bw Kang’ata, ambaye wakati huo alikuwa kiranja wa wengi katika Seneti, alimwandikia rais, alidai utafiti aliofanya ulibaini kati ya watu sita ni watu wawili pekee wanaunga mkono BBI.

Wandani wa Ruto katika kaunti ya Nakuru, wakiongozwa na Seneta Susan Kihika, nao walishindwa kuwashawishi madiwani kuangusha mswada huo kwani 62 waliuunga mkono. Ni madiwani 11 walipiga kura ya “LA”. Mswada huo ulipitishwa kwa kauli moja katika mabunge ya Narok na Bomet ambako idadi kubwa ya madiwani ni washirika wa karibu wa Dkt Ruto.

Sasa mswada huo utashughulikiwa na Bunge la Kitaifa na Seneti, kulingana na kipengele cha 257 cha Katiba ili kutoa nafasi kwa kura ya maamuzi.

Mapema Februari, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alisema kuwa Bunge la Kitaifa litahitaji muda wa wiki tatu pekee kujadili mswada huo.

Muturi alisema baada ya mswada huo kuchapishwa na bunge hilo, utapigwa msasa na kamati husika kabla ya kutajadiliwa kwenye kikao cha bunge lote.

“Baada ya mswada huo kupokewa rasmi bungeni, utachunguzwa na Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) kwa kushirikisha maoni ya umma. Baada ya hapo, bunge litahitaji majuma mawili au matatu kukamilisha mswada huo kwa sababu halina uwezo wa kuufanyia marekebisho,” akasema.

Bw Muturi alieleza kuwa, bunge la kitaifa halitahitaji kuushughulikia mswada huo kwa siku 90 inayohitajika kulingana na sheria za bunge kwani wananchi watapata fursa ya kuamua hatima yake katika kura ya maamuzi.

Hii ina maana huenda kura ya maamuzi ikafanyaka kabla ya Juni ilivyobashiriwa na Sekretariati ya BBI.

Jumanne, kiranja wa wachache Junet Mohammed ambaye ni mwenyekiti mwenza wa sekritarieti hiyo alisema wamepanga msururu wa mikutano ya hadhara kuanzia Machi 1 kuupigia debe mswada huo.

“Nilivyosema juzi, tumepanga msururu wa kampeni za kuuvumisha mswada huu wa BBI na kuwarai wananchi waupitishe katika kura ya maamuzi,” Bw Mohammed ambaye pia ni Mbunge wa Suna Mashariki.

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU