• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:20 AM
Bayern Munich waponda Lazio 4-1 kwenye mkondo wa kwanza wa 16-bora UEFA

Bayern Munich waponda Lazio 4-1 kwenye mkondo wa kwanza wa 16-bora UEFA

Na MASHIRIKA

JAMAL Musiala aliweka rekodi ya kuwa mwanasoka wa kwanza mchanga zaidi raia wa Uingereza kufunga bao kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) alipofungia Bayern Munich katika ushindi wa 4-1 uliosajiliwa na miamba hao dhidi ya Lazio mnamo Jumanne usiku jijini Roma, Italia.

Musiala, 17, alifunga bao la pili la waajiri wake katika dakika ya 24 na kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kucheka na nyavu za wapinzani akivalia jezi za Bayern kwenye soka ya UEFA.

Robert Lewandowski aliwafungulia Bayern ukurasa wa mabao katika dakika ya tisa kabla ya kiungo wa zamani wa Manchester City, Leroy Sane kufanya mambo 3-0 kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.

Francesco Acerbi wa Lazio alijifunga katika dakika ya 47 na kuwapa Bayern bao la nne kabla ya Joaquin Correa kuwafutia waajiri wake machozi sekunde chache baadaye.

Goli la Lewandowski ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Bayern lilikuwa lake la 72. Nyota huyo sasa amempiku aliyekuwa fowadi matata wa Real Madrid na Schalke, Raul Gonzalez na kuwa mwanasoka wa tatu baada ya Cristiano Ronaldo wa Juventus na Lionel Messi wa Barcelona wanaojivunia idadi kubwa zaidi ya mabao kwenye kipute cha UEFA. Kufikia sasa, Ronaldo ametikisa nyavu za wapinzani mara 134 huku Messi akifunga magoli 119 kwenye soka ya bara Ulaya.

Bayern ambao pia ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), walitia kapuni ufalme wa Kombe la Dunia wiki chache zilizopita baada ya kuwafunga Tigres UANL ya Mexico 1-0 kwenye fainali iliyowakutanisha nchini Qatar. Kikosi hicho cha kocha Hansi Flick sasa kimejizolea jumla ya mataji sita chini ya kipindi cha miezi tisa iliyopita.

Japo ni raia wa Uingereza, Musiala yuko huru kuteua kuchezea timu hiyo ya kocha Gareth Southgate au kikosi cha Ujerumani ambacho kwa sasa kinatiwa makali na mkufunzi Joachim Loew.

Kwa kufunga bao dhidi ya Lazio kwenye UEFA, Musiala alivunja rekodi ya kiungo wa sasa wa Liverpool, Alex Oxlade-Chamberlain aliyewahi kufungia Arsenal bao la UEFA dhidi ya Olympiakos ya Ugiriki mnamo Septemba 2011 akiwa na umri wa miaka 18 na siku 44 pekee. Hadi kufikia Februari 23, Oxlade-Chamberlain ndiye alikuwa Mwingereza mchanga zaidi kuwahi kufunga bao kwenye kivumbi cha UEFA.

Hii ni mara ya kwanza kwa Lazio kufikia hatua ya 16-bora kwenye soka ya UEFA. Kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kitarudiana na Bayern uwanjani Allianz Arena mnamo Machi 17, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Musau Muia

Nafasi ipo kuimarisha BBI iwafae Wakenya – Mudavadi