• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
KINA CHA FIKIRA: Punguza mizigo mizito inayoweza kukuweka pabaya katika maisha

KINA CHA FIKIRA: Punguza mizigo mizito inayoweza kukuweka pabaya katika maisha

Na WALLAH BIN WALLAH

WATU wenye busara na hekima walisema kwamba huwezi kuukwea mti mrefu kuenda kileleni ukiwa umebeba mizigo mizito kichwani, mabegani na mgongoni!

Utalemewa na uzito uvutwe uanguke chini badala ya kuenda juu! Ni vizuri kuepuka kikwazo chochote kinachoweza kukuzuia kusonga mbele ili utimize malengo yako uliyodhamiria maishani. Punguza mizigo ili uivuke bahari bila kuzama kwenye mawimbi makali.

Naam, hebu niitumie fursa hii adhimu kuwakumbusha na kuwashauri wanafunzi wetu wapendwa walio shuleni kwamba kusoma ni sawa na kuukwea mti mrefu kuenda kuyatafuta matunda ya kula baadaye maishani! Kila hatua ya masomo shuleni ni mfano wa hatua za kunyanyua miguu kuukwea mti kuenda kileleni kuyaangua matunda matamu ambayo hayajagugunwa na mayonda na ngedere wa porini! Lakini ni vigumu zaidi kuukwea mti ukiwa na mizigo mingi mizito inayokulemea mwilini. Utashindwa! Hatimaye utaanguka chini pamoja na mizigo yako ikuporomokee ikuumize pale pale chini ulopoangukia pu!! Kwa hivyo lazima upunguze mizigo au uache kabisa mizigo yote mizito chini upande juu ya mti uyaangue matunda ndipo ushuke chini uichukue mizigo yako endapo utakuwa na haja nayo!

Ninasema endapo utakuwa na haja nayo kwa sababu labda mizigo uliyokuwa uking’ang’ana kuibeba haikuwa na umuhimu au thamani yoyote kubwa kuliko matunda uliyoyapata juu ya mti ulioukwea! Masomo ni matunda na shule ni mti. Soma uyapate matunda ya masomo badala ya kujibebesha mizigo mingi mizito inayoweza kukuzuia na kukukwaza katika masomo yako kama vile kujibebesha mizigo ya kuvuta sigara na bangi shuleni! Au mizigo ya kuwa na utovu wa nidhamu kutorokatoroka shuleni kuenda kutafuta starehe za paka kunawa uso kwa kutumia mate! Ama mzigo wa kichaa cha mbwa alicho nacho ngedere kuamua kuchoma moto msitu na miti yote ambayo ndiyo maskani yake na pia ndiyo inayompa matunda anayokula! Mwanafunzi anayefikiria kuchoma shule mahali anaposomea, ametumia akili gani kufikiri? Ama kweli, kufikiri ni kazi!!

Ukitaka kuivuka bahari ya maisha, upunguze mizigo mingi uliyoijaza katika jahazi kabla ya jahazi kuzama! Na ukitaka kuukwea mti uende juu kuyaangua matunda, uiache mizigo chini. Ni masikitiko makubwa kuona kwamba mwanafunzi anayesomea shuleni kuyatafuta maisha ya baadaye, anachagua kufukuzwa kutoka shuleni ati kwa sababu hana nidhamu, hataki kusoma! Anadai chakula kizuri shuleni lakini hataki kunyolewa nywele na ndevu!!? Ati anataka asome akiwa na nywele za misokoto na ndevu kama za Joseph Kasavuvu?! Punguza mizigo ya upuuzi ili uyapate maisha mazuri ya siku zijazo!!!

You can share this post!

NASAHA: Chukua hatua kuimarisha kumbukumbu yako...

Mradi wa ujenzi wa kituo cha elimu na mafunzo kukabiliana...