Raila achangamkia kupitishwa kwa BBI

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Waziri Mkuu Raila Odinga amewamiminia sifa madiwani kufuatia hatua ya mabunge 26 ya kaunti kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba kupitia mapendekezo ya ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI).

Bw Odinga alisema hatua ya mabunge ya kaunti sasa imeongeza matumaini ya Wakenya kushiriki kura ya maamuzi ambayo imeratibiwa kufanyika Juni 2021.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, kiongozi huyo wa ODM alisema kuwa licha ya yale aliyoyataja kama propaganda na habari za kupotosha zinazosambazwa kuhusiana na mageuzi ya Katiba, mabunge ya kaunti yamesimama thabiti.

“Mabunge ya kaunti yameweza kuweka kando kampeni za mwaka mmoja za uwongo kuhusu stakabadhi hii inayolenga kuhakikisha kuwa Kenya inapiga hatua kimaendeleo katika nyanja zote,” akasema Bw Odinga.

“Nawapongeza madiwani wetu na magavana ambao walikataa kukubali uvumi uliokuwa ukienezwa na wapinzani wa BBI na wakaupitisha mswada huo kwa kauli moja,” akaongeza.

Mnamo Jumanne jumla ya mabunge ya kaunti 26 yalipitishwa mswada huo wa BBI na kufikisha 38 idadi ya mabunge ya kaunti ambayo yamefanya hivyo. Kufikia Jumatatu wiki hii ni mabunge 12 yalikuwa yamepitisha mswada huo.

Kwa hivyo, kufikia Jumanne kaunti 38 zilikuwa zimepitisha mswada huo. Kaunti hizo ni pamoja na; Siaya, Kisumu, Homa Bay, Migori, Busia, Kakamega, Bungoma, Trans Nzoia, Vihiga, Pokot Magharibi, Nakuru, Nairobi, Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga na Kiambu.

Kaunti zingine ni; Meru, Nyamira, Narok, Kajiado, Taita Taveta, Kitui, Makueni, Lamu, Mombasa, Kwale, Garissa, Machakos, Muranga, Samburu, Marsabit, Kisii, Tana River, Samburu, Kwale, na Marsabit.

Kericho imepitisha mswada huo.

Kaunti saba ambazo hazijajadili mswada huo ni pamoja na Kilifi, Wajir, Mandera, Uasin Gishu, Nandi, Elgeyo Marakwet na Turkana. Ni kaunti ya Baringo pekee imekataa mswada huo.

Habari zinazohusiana na hii

UHURU AMTULIZA RAILA

Wababaisha ‘Baba’

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Kichwa kinauma

Raila akausha marafiki