• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Mradi wa ujenzi wa kituo cha elimu na mafunzo kukabiliana na itikadi kali na ugaidi wazinduliwa Lamu

Mradi wa ujenzi wa kituo cha elimu na mafunzo kukabiliana na itikadi kali na ugaidi wazinduliwa Lamu

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI imezindua mradi wa Sh347 milioni wa ujenzi wa kituo maalum cha elimu na taasisi ya kiufundi kusaidia kuwanasua vijana kutoka kwa itikadi kali na ugaidi kwenye msitu wa Boni.

Mradi huo ambao ukikamilika utawawezesha vijana wa vijiji vya msitu wa Boni kupokezwa elimu na ujuzi.

Unatekelezwa kwenye eneo la Bar’goni, tarafa ya Hindi, Kaunti ya Lamu.

Akihutubia umma wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo kijijini Bar’goni, Mwenyekiti wa Tume ya Kuajiri Polisi nchini (NPSC), Eliud Kinuthia, alitaja Lamu na Kwale kuwa kaunti ambazo serikali ilizipa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Alisema vijana wengi kwenye kaunti hizo mbili kwa miaka mingi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za itikadi kali na kuishia kusajiliwa kuingia makundi ya uhalifu, ikiwemo al-Shabaab.

Mwenyekiti wa Tume ya Kuajiri Polisi Nchini (NPSC), Eliud Kinuthia akihutubia umma kijijini Bar’goni kabla ya kuzindua kituo maalum cha elimu kukabiliana na itikadi kali. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Kinuthia alisema mbali na serikali kuendeleza operesheni ya usalama ya Linda Boni kwenye msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu, ilionelea vyema kwamba mbinu mbadala ambayo ni kuwapa vijana elimu izinduliwe ili kusaidia kufaulisha harakati za kumaliza ugaidi miongoni mwa jamii.

Alisema mradi wa ujenzi wa shule hiyo maalum ya upili na chuo cha kiufundi kijijini Bar’goni unatarajiwa kuchukua muda wa miaka miwili kabla ya kukamilika.

Tayari mwanakandarasi aliyepata zabuni ya mradi huo amepewa siku 90 kukamilisha, ambapo serikali imetoa Sh 10 milioni kwa utekelezaji na kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo.

“Leo tuko hapa Bar’goni kuzindua rasmi ujenzi wa shule maalum ya upili na chou cha kiufundi. Lengo la mradi huu ambao utagharimu serikali Sh 347 milioni ukikamilika ni kupanua eneo hili la operesheni na kuwanasua vijana kutoka kwa itikadi kali na ugaidi kupitia elimu. Ningeomba jamii kushirikiana na serikali ili kufaulisha mpango huu,” akasema Bw Kinuthia.

Mbunge wa Lamu Magharibi, Stanley Muthama alitaja mradi huo kuwa mwamko mpya hasa kwa jamii ndogo ya Waboni ambayo imekuwa ikilalamika kuhusiana na hali duni ya elimu vijijini mwao.

Bw Muthama aliwataka wananchi, hasa Waboni kujitolea na kuwapeleka Watoto wao shuleni na vyuoni wasome ili wasaidie kubadilisha Maisha ya jamii hiyo ndogo.

“Namshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kuchagua Lamu kuwa miongoni mwa kaunti zenye kunufaika na mpango huo wa kituo maalum cha elimu na chou cha kiufundi. Eneo la Waboni limekuwa na changamoto tele za elimu kutokana na utovu wa usalama unaochangiwa na al-Shabaab. Nashukuru kwamba eneo hili la msitu wa Boni ni salama na maendeleo yanazidi kuafikiwa hapa,” akasema Bw Muthama.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia alimhakikishia mwanakandarasi usalama wa kutosha wakati akitekeleza mradi huo.

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Punguza mizigo mizito inayoweza kukuweka...

Mudavadi asisitiza NASA iko kwenye chumba mahututi cha...