• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Wazazi washauriwa kuangazia majukumu yao

Wazazi washauriwa kuangazia majukumu yao

Na LAWRENCE ONGARO

WAZAZI wanapitia changamoto tele katika maswala ya malezi na kwa hivyo ni vyema kupata mawaidha ya kila mara ili kukabiliana nazo.

Kanisa la Glory Outreach Assemblies (GOA) lililoko Kahawa Wendani limejitolea kufanya mikutano ya kila mara ili kuwahamasisha wazazi jinsi ya kukaa vyema na watoto wao wanapokuwa nyumbani.

Askofu mkuu wa kanisa hilo Bw David Munyiri, mnamo Jumatatu katika semina moja alisema kanisa lina jukumu kubwa la kuhamasisha wazazi namna ya kukabiliana na changamoto hizo za wana wao.

“Tunataka kuona ya kwamba kanisa linachukua mstari wa mbele kuwapa wazazi mawaidha ya jinsi wanavyoweza kukaa na watoto wao. Wazazi nao ni lazima wawajibike ipasavyo wakati wa malezi,” alisema Bw Munyiri.

Alisema hata watoto nao wanasongwa na mambo mengi akilini kwa sababu utapata watoto wakija kanisani kudai kuwa mwalimu wake alimtukana na kwa hiyo ni njia mbovu ya kumkuza mwanafunzi ukiwa mwalimu.

Aliongeza kusema ya kwamba wazazi wawe na wakati wa kuzungumza na watoto wao kwa sababu imebainika ya kwamba wazazi wengi wanahusudu kazi kuliko maswala ya familia.

“Kila mzazi ana jukumu la kuchukua muda wake kumuelewa mtoto wake vyema ili kujua matatizo yake. Hii inahitaji ushirikiano mwema na upendo,” alisema mchungaji huyo.

Mwanasaikolojia Bi Truphena Wakaba alisema wanafunzi wengi wametekwa nyara na simu za rununu na mitandao ya mawasiliano.

“Kwa hivyo wazazi wanastahili kufuatilia kwa makini ni mambo gani ambayo watoto hao wanafuatilia kwa simu zao na katika mitandao. Sio vyema kumkataza kutumia vifaa hivyo lakini cha muhimu ni kumuelimisha hatari iliyopo iwapo atatumia visivyo kifaa hicho,” alisema Bi Wakaba.

Alisema ni vyema kuelewa mazingira ya watoto hao na kufuatilia kila mara mambo wanayofanya na wenzao.

Mshikadau wa kielimu Bi Lizzie Wanyoike alisema utovu wa nidhamu umekithiri akipendekeza kiboko kinastahili kurejeshwa shuleni “lakini walimu wawe makini kukitumia.”

“Tunataka kuona watoto wenye nidhamu wala sio watundu ambao wanatenda mambo yao kutokana na hisia za wanafunzi wenzao,” alisema Bi Wanyoike.

Naye Bi Sophia Wanjiru ambaye ni mzazi alisema kanisa ni pahala pazuri pa kutafuta ushauri kwani siku hizi mambo yamevuka mipaka.

“Tunajua kanisa ndipo pahala pazuri pa kupata mawaidha kutoka kwa wachungaji na hapo ndipo pia maswala ya kifamilia yanapatikana. Kwa hivyo sisi kama wazazi tuwe mstari wa mbele kutekeleza wajibu wetu wa kulea watoto jinsi ipasavyo,” alisema Bi Wanjiru.

You can share this post!

BBI: Raila apinga wazo la kura ya maamuzi kuandaliwa pamoja...

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 280 idadi jumla...