Raila amtia Ruto pancha

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, Jumatano aliwashukuru madiwani wa mabunge ya kaunti waliopitisha mswada wa marekebisho ya katiba wa BBI akisema kwamba “walimtoa pumzi” Naibu Rais, Dkt William Ruto na washirika wake.

Kufikia jana, mabunge 40 ya kaunti yalikuwa yamepitisha mswada huo ikiwa ni 16 zaidi ya idadi inayohitajika kikatiba ya mabunge 24 kati ya 47.

Miongoni mwa kaunti hizo ni ngome za Naibu Rais William Ruto ambaye amekuwa akiongoza washirika wake kukosoa mchakato wa kubadilisha katiba.

Baadhi ya kaunti hizo ni Bomet iliyopitisha mswada huo Jumanne na Kericho na Turkana ambazo ziliupitisha jana.

Dkt Ruto na wandani wake walikuwa wameapa kuzima mchakato wa kura ya maamuzi wakisema wanachohitaji Wakenya kwa wakati huu ni mikakati ya kuinua hali yao ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Bw Odinga amekuwa akitaja kampeni ya Dkt Ruto kama taka akisema mabadiliko ya katiba yanatoa mazingira bora ya amani na uchumi.

Jumatano akiwa mwingi wa bashasha, Bw Odinga alisema kwamba madiwani walionyesha uzalendo licha ya presha kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wakatae mswada huo.

Alisema kwa kufanya hivyo, madiwani walimuonyesha Dkt Ruto kuwa Wakenya si watu wajinga wanaoweza kupotoshwa.

“Tuna furaha kwamba tumeona mwangaza, Wakenya wamezungumza, tena kwa sauti kubwa,” alisema akihutubia vijana kutoka kaunti za eneo la Mashariki jijini Nairobi.

Alisema wale waliokuwa wameapa kuzima mchakato wa kubadilisha katiba wameaibika na kubaini kwamba Wakenya wanaweza kufanya uamuzi unaofaa kuhusu nchi yao.

“Walikuwa wakijifanya wao ndio wanajua kuongea na Wakenya lakini mimi ninasema Wakenya ni werevu. Walikuwa wanafikiri Wakenya ni takataka yao kumbe wanacheka na kukupigia makofi unadhani wako nawe,” alisema.

Dkt Ruto na washirika wake wa kisiasa wamekuwa wakiandaa mikutano mikubwa ya hadhara ambayo wamekuwa wakikosoa mswada wa marekebisho ya katiba wa BBI. Bw Odinga alisema licha ya Dkt Ruto kukosoa mchakato huo, Wakenya wameonyesha kuwa wanajua kufanya maamuzi yanayofaa.

“Wanaweza kukupigia makofi ukafikiri wewe ni mwerevu sana lakini wakati unaofaa ukifika, Wakenya wanajua kufanya uamuzi wao,” alisema.

Bw Odinga aliwaambia vijana waunge mswada huo akisema mabadiliko ya katiba yanayopendekezwa kupitia mswada huo yatawahakikishia maisha na nchi bora.

“Tunataka vijana wawajibike, tutembee nao katika safari hii ya kumaliza ukabila ili waweze kuwa na maisha bora. Ukabila ulizaliwa na viongozi si wananchi na tunataka kuumaliza,” akasema.

“Vijana ndio wanafaa kubeba jukumu la kukomboa nchi hii. Tunataka kubadilisha akili na mawazo ya Wakenya. Tunachotaka ni mabadiliko, tunataka nchi ambayo waanzilishi wa taifa hili walitaka, nchi bila ukabila,” alisema.

Alipuuza madai ya wandani wa Dkt Ruto kwamba eneo la Mlima Kenya ambalo ni ngome ya Rais Kenyatta haliwezi kumuunga mkono.

“Eti walisema Raila hawezi kutembelea Mlima Kenya. Waongo, mimi nina nguvu hata za kupanda na kushuka milima na mabonde,” alitania.

Katika mipango ya kuzima kampeni ya Dkt Ruto ambayo alilenga vijana katika juhudi za kuzima mchakato huo, Rais Uhuru Kenyatta alisema mabadiliko ya katiba yataimarisha mazingira ya kufanya biashara.

Akihutubia vijana katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Nairobi wakati wa kutoa zawadi kwa washindi wa shindano la kibiashara la MbeleNakazi lililoanzishwa na serikali kuwanufaisha zaidi ya vijana 250,000, Rais Kenyatta alisema mabadiliko ya katiba yananuiwa kuwafaidi.

Kulingana na kamati inayosimamia mchakato huo, Rais Kenyatta na Bw Odinga, wataongoza kampeni za kuvumisha mswada wa BBI kote nchini kuanzia Machi.

Kampeni hizo zinanuiwa kuzima kampeni ya Dkt Ruto ambaye hadi wakati wa kwenda mitamboni jana hakuwa amezungumzia hatua ya kupitishwa kwake na mabunge ya kaunti.

Habari zinazohusiana na hii

UHURU AMTULIZA RAILA

Wababaisha ‘Baba’

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Kichwa kinauma

Raila akausha marafiki