• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
Messi afunga mabao mawili na kusaidia Barcelona kupepeta Elche 3-0 La Liga

Messi afunga mabao mawili na kusaidia Barcelona kupepeta Elche 3-0 La Liga

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alifunga mabao mawili na kusaidia waajiri wake Barcelona kupepeta Elche 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumatano usiku.

Ushindi huo ulisaidia kikosi hicho cha kocha Ronald Koeman kupunguza pengo la alama kati yao na viongozi wa jedwali Atletico Madrid hadi pointi tano pekee.

Barcelona kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 50, mbili nyuma ya nambari mbili Real Madrid ambao ni mabingwa watetezi. Hata hivyo, nafuu zaidi kwa Atletico wanaotiwa makali na kocha Diego Simeone, ni kwamba wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo tayari zimepigwa na washindani wao wakuu wakiwemo Real na Barcelona.

Sevilla ambao wamecheza idadi sawa ya michuano na Atletico (23), wanafunga orodha ya nne-bora jedwalini kwa alama 48.

Messi, 33, aliwafungulia Barcelona ukurasa wa mabao katika dakika ya 48 baada ya kukamilisha krosi safi aliyopokezwa na fowadi raia wa Denmark, Martin Braithwaite.

Mshambuliaji na nahodha huyo raia wa Argentina alipachika wavuni bao la pili la Barcelona katika dakika ya 68 baada ya kushirikiana vilivyo na beki raia wa Uholanzi, Frenkie de Jong.

Jordi Alba alizamisha kabisa chombo cha Elche katika dakika ya 73 baada ya kupokezwa pasi nzuri na Braithwaite. Messi kwa sasa ametitiga nyavu za wapinzani mara 18 kufikia sasa kwenye kampeni za La Liga msimu huu na ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji bora kwa magoli mawili zaidi kuliko Luis Suarez wa Atletico.

Suarez ambaye pia amewahi kuchezea Liverpool, aliagana na Barcelona mwishoni mwa msimu uliopita wa 2019-20.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Onyo kwa makanisa yakome kuombaomba pesa za wanasiasa

Asilimia 24 ya Wakenya hatarini kufa njaa