• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 7:55 AM
Asilimia 24 ya Wakenya hatarini kufa njaa

Asilimia 24 ya Wakenya hatarini kufa njaa

Na BENSON MATHEKA

KENYA imeorodheshwa ya 84 miongoni mwa nchi 107 ulimwenguni ambazo raia wake wanakabiliwa na hali hatari ya njaa.

Hali hii imesababisha asilimia 23.7 ya raia wote humu nchini hukosa lishe bora, watoto kudumaa katika ukuaji na hali mbaya ya afya ya waathiriwa.

Kulingana na ripoti ya hali ya njaa ulimwenguni, ya mwaka 2020 iliyotolewa Jumatano, Kenya inakabiliwa na wakati mgumu kumaliza njaa miongoni mwa raia wake na kutoa lishe bora kabla ya 2030.

Waandalizi wa ripoti ya Global Hunger Index wanasema kwamba miaka ya maisha ya Wakenya inatarajiwa kupungua kwa sababu ya kukosa chakula na lishe bora.

Ripoti hiyo inasema kwamba ingawa Kenya imepiga hatua katika kukabiliana na hali ya njaa kutoka nambari 86 mwaka 2019 hadi 84 mwaka 2020, hatua zaidi zinahitajika kuokoa raia hasa watoto wanaokosa kukua vyema.

Ripoti inaeleza kwamba asilimia 31.1 ya watoto nchini hudumaa kwa sababu ya njaa na ukosefu wa lishe bora, asilimia 4.9 wana uzani uliopungua ikilinganishwa na miaka yao na asilimia 4.1 hufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano kwa sababu ya njaa.

“Watoto ndio huathiriwa zaidi na ukosefu wa chakula cha kutosha, wanakosa kukua vyema, kuwa na uzani uliopungua na kufa,” alisema Kelvin Shingles mkurugenzi wa shirika la Welt Hunger Hifle lililoandaa ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano.

Hali hii mbaya zaidi katika kaunti kame vile Kitui na Pokot Magharibi ambapo ripoti inasema asilimia 40 ya watoto hawakui vyema.

Japo awali hali hii ilihusishwa na uhaba wa mvua na mabadiliko ya tabianchi, ripoti hiyo inasema inaweza kuwa mbaya zaidi mwaka huu kufuatia athari za janga la corona na uvamizi wa nzige.

“Ripoti hii haikuhusisha athari za corona na inatarajiwa itachangia pakubwa kuzidisha athari za njaa,” inasema ripoti hiyo.

Inasema serikali inafaa kuweka sera na mikakati thabiti ya kuimarisha utoshelevu wa chakula ili kuepusha raia dhidi ya njaa na kuimarisha afya.

Kulingana na katibu wa wizara ya Kilimo Prof Hamadi Boga, serikali imechukua hatua za kuhakikisha utoshelevu wa chakula nchini kupitia miradi mbalimbali.

Ripoti hiyo inatolewa wakati Wakenya wakiendelea kukabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na ushuru wa juu na janga la corona.

You can share this post!

Messi afunga mabao mawili na kusaidia Barcelona kupepeta...

Alipata tenda ya Sh1.3bn miezi 2 baada ya kusajili kampuni