TAHARIRI: Serikali iifuatilie ripoti kuhusu njaa

KITENGO CHA UHARIRI

SHIRIKA moja la kigeni limetoa ripoti ya hali ya njaa ulimwenguni na Kenya haijakuwa pahali salama.

Ripoti ya Global Hunger Index inasema kwamba ingawa Kenya imepiga hatua katika kukabiliana na hali ya njaa kutoka nambari 86 mwaka 2019 hadi 84 mwaka jana, hatua zaidi zinahitajika kuokoa raia, hasa watoto wanaokosa kukua vyema.

Inaeleza kwamba Kenya inakabiliwa na wakati mgumu kumaliza njaa miongoni mwa raia wake na kutoa lishe bora kabla ya 2030.

Kuwa na chakula cha kutosha na kujisimamia kwa lishe ni mojawapo ya maono ya maendeleo kwenye Ruwaza ya mwaka 2030. Maono hayo huenda yakabakia kuwa ndoto tu, iwapo ufichuzi wa ripoti hiyo hautaanza kushughulikiwa.

Tayari ripoti inaonyesha kuwa hali ni mbaya sana katika kaunti kame vile Kitui na Pokot Magharibi, ambako karibu nusu ya watoto hawakui inavyotakikana kwa sababu ya kukosa chakula bora na cha kutosha.

Ripoti hii inaeleza hali ilivyokuwa hata kabla ya kuingia nchini kwa janga la corona na kuendelea kuzagaa kwa nzige. Ugonjwa huo ulisababisha kufungwa kwa shughuli mbalimbali. Kuna wakati serikali iliamuru kila mtu akae ndani ya nyumba, wakiwemo wakulima.

Na wale wakulima wachache ambao walikuwa wametangulia kupanda kabla ya kuzuka kwa janga hilo, walipoteza matumaini na wakakosa mavuno baada ya wingu la nzige kuvamia karibu kaunti 40.

Serikali inapaswa kuchukua jukumu la kuwasaidia wakulima kurejelea hali ya kawaida kwa kuweka sera na mikakati ya kuimarisha utoshelevu wa chakula, ili kuepusha raia dhidi ya njaa na kuimarisha afya.

Njia moja ya haraka ya kufanya hivyo ni kuwaepushia wakulima madalali wanaouza mbolea aina ya DAP kwa bei ya juu.

Mwaka jana Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya aliwaahidi wakulima kwamba wangeuziwa mbolea ya bei nafuu kutoka kwa viwanda kupitia kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).

Lakini sasa wasambazaji mbolea wameongeza bei kutoka Sh2,300 hadi Sh3,200 na kufanya shughuli ya kilimo kuwa ghali.

Serikali pia yaweza kuwapeleka maafisa wa kilimo nyanjani, ili kuwafunza wakulima jinsi ya kuimarisha mazao.

Habari zinazohusiana na hii