KINYUA BIN KING’ORI: Viongozi wamegeuza taifa kupiga siasa kila wakati

Na KINYUA BIN KING’ORI

WANASIASA wanaozunguka kila siku wakipiga kampeni za urais 2022 wanafaa kutumia muda huo kusaidia wananchi walalahoi kusuluhisha matatizo yanayowakumba maishani.

Hatua ya hata viongozi wakuu serikalini na kaunti kuepuka majukumu yao muhimu na kufanya kampeni za 2022, inakera.

Badala ya viongozi hao kushirikiana na serikali kutekeleza miradi inayoweza kusaidia uchumi wetu kuimarika, ajira kupatikana na maendeleo kuboreshwa, wao wanalenga tu siasa na kampeni ambazo haziwezi kumfaa mwananchi wa kawaida.

Miongoni mwa vigogo ambao wameishi kujivumisha siasa kabla ya 2022 ni Naibu Rais Dkt William Ruto, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Alfred Mutua na Gideon Moi.

Wanasiasa hao wanatumia pesa nyingi mno kuzunguka huku na kule kufanya kampeni za mapema utadhani uchaguzi mkuu ni mwaka huu.

Iwapo fedha wanazofanyia kampeni wangeziekeza katika miradi muhimu ya maendeleo huku wakieleza wananchi sera zao zitakazowafaidi, tungalikuwa na matumaini ya kupata viongozi bora na serikali nzuri baada ya uchaguzi mkuu 2022.

Japo wanasiasa wana haki ya kupiga siasa, wafahamu kampeni za 2022 zina wakati wake.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ndiyo yenye mamlaka kutangaza rasmi kuanza kwa kampeni; wanaozifanya sasa hivi wakilenga uchaguzi wa 2022 wanavunja sheria.

Wanasiasa wakuu wakikosa kudhibitiwa tamaa yao ya kujitafutia mamlaka mapema hii, basi wajue wataumiza nchi kiuchumi, kiusalama, kijamii na kisiasa.

Kwa sababu ya siasa za mapema, uchumi wa taifa unayumbayumba baada ya viongozi kuweka maendeleo pembeni na kuelekeza rasilimali na muda katika siasa za urithi na mchakato wa kubadlisha Katiba kupitia Mswada wa BBI.

Viongozi wanapopiga siasa wananchi wanakorogwa na kutumiwa kama makundi ya kuzua vurugu katika mikutano ya kisiasa au kwenye hafla za mazishi, wakilenga kuonyeshana ubabe na jinsi walivyo na umaarufu katika maeneo mbalimbali nchini.

Hatuwezi kuwa taifa lenye kuweka siasa kipaumbele kila wakati huku tukisahau mateso, usumbufu na mahangaiko wanayopitia wananchi wa kawaida kusaka riziki ya siku tu moja bila mafanikio.

Ni vigumu mno raia kufaulu katika taifa ambalo viongozi wake wanaishi kuzozana kufanya malumbano ya siasa za urithi miaka miwili au mitatu kabla ya kipindi rasmi cha kampeni kutangazwa.

Tunafaa tuige mataifa jirani, kwa mfano nchi ya Tanzania, ambayo baada ya kura kukamilika viongozi waliochaguliwa wanatumia muda, nguvu na rasilimali kustawisha nchi yao.

Wale hawakufanikiwa kuchaguliwa nao wamechukua jukumu la kukosoa serikali hadi kipindi kijacho cha kampeni za uchaguzi mwingine kifike, bila kujivumisha au kusaka mbinu za kiujanja kujumuishwa serikalini.

Tubadilishe mbinu zetu za kisiasa, na wanasiasa wote wakomeshe kampeni hizi za mapema.

Badala yake waungane kuhakikisha miradi ya maendeleo kwa umma imetekelezwa na kukamilishwa bila kuchelewa.

Habari zinazohusiana na hii