KAMAU: Teknolojia: Afrika isisingizie wakoloni kuachwa nyuma

Na WANDERI KAMAU

UKUAJI wa teknolojia duniani ulichangiwa pakubwa na Enzi ya Uvumbuzi barani Ulaya, iliyojiri kati ya karne ya 14 na 17.

Wakati huo, masuala mengi yaliyohusu maisha ya jamii yalibadilika sana.

Mabadiliko hayo yalitokana na mchipuko wa kizazi kipya cha kiusomi, ambacho kilichangia sana uvumbuzi katika karibu nyanja zote.

Miongoni mwa nyanja zilizoshuhudia mageuzi ni falsafa, fasihi, sanaa na ufundi wa mitambo.

Ni wakati huo ambapo waandishi maarufu kama William Shakespeare walichipuka.

Vile vile, ni nyakati hizo ambapo wavumbuzi maarufu kama Galileo Galilei na Jethro Tull kati ya wengine walichipuka, na kuchangia pakubwa katika ukuaji wa sayansi ya masuala ya angani na ufundi wa mitambo.

Bila shaka, enzi hiyo ndiyo iliweka msingi na kuchochea ueneaji wa ujuzi huo katika maeneo mengine duniani kama Asia, Amerika, Afika na kwingineko.

Ingawa ujuzi huo ulienea na kukumbatiwa haraka katika maeneo kama Amerika, hali ilikuwa kinyume barani Afrika.

Ujio wa wakoloni uligeuka kuwa kikwazo kikubwa kwa jamii za Kiafrika kupata maarifa hayo mapya.

Kosa kuu ambalo wakoloni walifanya ni kuwazuia Waafrika kufaidika kwa maarifa hayo; wengi wao walihofia huenda wakawageuka ikiwa wangepata nafasi yoyote ile kuerevuka.

Kosa kubwa ambalo Waafrika walifanya ni kukubali “uduni” waliorushiwa na wakoloni; wengi wao walikubali na kukumbatia dhana ya kutokuwa werevu na wenye ujuzi ikilinganishwa na Wazungu.

Hadi sasa, dhana hiyo ndiyo imekuwa kikwazo kwa nchi nyingi barani humu kustawi na kuendesha uvumbuzi katika masuala ya teknolojia.

Inasikitisha kuwa zaidi ya nusu karne tangu mataifa hayo kujinyakulia uhuru, mengi bado yanaendelea kubaki nyuma kiteknolojia, wakati nchi zingine zinaendesha karibu shughuli zake zote muhimu kwa teknolojia!

Mataifa mengi Afrika bado yanaogelea kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, wakati nchi kama Amerika zinafanya majaribio kubaini ikiwa mwanadamu anaweza kuishi katika Sayari Mirihi (Mars).

Alhamisi iliyopita, Amerika ilifanikiwa kutuma kifaa maalum cha kuzuru angani (Perserverence Rover) katika Sayari Mirihi, kutathmini tena iwapo kuna uwezekano wa mwanadamu kuishi huko.

Ijapokuwa kifaa hicho si cha kwanza kutumwa katika sayari hiyo, upekee wa mtambo huo mara hii ni kwamba umetengenezwa kwa ustadi mkubwa wa kiteknolojia.

Kifaa hicho kilianza kurusha picha duniani mara tu baada ya kufika kwenye sayari.

Bila shaka, mielekeo kama hiyo inapaswa kuwa changamoto kwa serikali na viongozi wa Afrika kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika teknolojia.

Licha ya mafanikio hayo, Amerika imepitia changamoto sawa na nchi nyingi za Afrika.

Kama Afrika, Amerika ilikuwa koloni ya Uingereza hadi pale ilipojipatia uhuru mnamo 1776.

Vile vile, sawa na mataifa mengi barani humu, ilikumbwa na vita vya majimbo ya Kusini na Kaskazini kati ya 1861 na 1865.

Mbona Afrika isijifunze kutoka kwa Amerika? Ni kosa kuu kwa Afrika kuendelea kulalamikia “ukoloni” kuwa chanzo cha kuachwa nyuma kiteknolojia.

akamau@ke.nationmedia.com

Habari zinazohusiana na hii