• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Serikali yaahidi kusaidia Kenya Morans kujiandaa kwa AfroBasket

Serikali yaahidi kusaidia Kenya Morans kujiandaa kwa AfroBasket

Na GEOFFREY ANENE

WAZIRI wa Michezo Amina Mohamed ameahidi kuwa serikali itasaidia kikamilifu timu ya taifa ya mpira ya vikapu ya wanaume, Kenya Morans, kujiandaa kwa Kombe la Bara Afrika (AfroBasket).

Morans ya kocha Elizabeth Mills ilishinda michuano miwili kati ya sita iliyocheza katika kampeni za kufuzu ikiwemo kuangusha miamba Angola na kujikatia tiketi ya kuwa AfroBasket baadaye mwaka 2021 nchini Rwanda. Ni mara ya kwanza kabisa Morans imefuzu kushiriki dimba hilo tangu Kenya iwe mwenyeji mwaka 1993 ilipokamilisha katika nafasi ya nne.

Akizungumza katika dhifa ya chakula cha mchana ya timu hiyo baada ya washindi hao medali ya fedha ya AfroCan 2019 kurejea nyumbani kutoka Cameroon, Amina alisema kuwa “Wizara itasaidia Morans kuwa kambini kabla ya AfroBasket jijini Kigali na pia kulipia gharama ya kushiriki dimba hilo”.

“Tutahakikisha kuwa mahitaji yote ya mazoezi ya timu na mashindano yanashughulikiwa kwa muda unaofaa,” alisema waziri huyo ambaye alikiri kuwa ilikuwa heshima kubwa kuwa pamoja na timu hiyo kula chakula cha mchana na kusherehekea ushindi huo wa kihistoria uliohakikishia Kenya tiketi ya kushiriki AfroBasket itakayokutanisha mataifa 16.

Amina alishukuru sekta ya kibinafsi pia kuungana na serikali kusaidia Morans na akaomba wadhamini zaidi wajitokeze kuinua mpira wa vikapu na michezo kwa jumla.

“Nachukua fursa hii pia kushukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kuona mbele alipoanzisha mfuko wa kufadhili timu zote za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa,” alihitimisha.

Morans ilianza kampeni ya kuingia AfroBasket kwa kupepeta Eritrea 112-64, Tanzania 95-59, Somalia 102-77, Burundi 101-83 na Sudan Kusini 74-68 mwezi Januari 2020 katika Kundi D la kufuzu kushiriki awamu ya mwisho.

Katika awamu ya mwisho ya kuingia AfroBasket, ambayo iligawanywa katika madirisha mawili, Kenya ilibwagwa na Senegal 92-54 na Angola 75-52 na kunyamazisha Msumbiji 79-62 katika dirisha la kwanza mnamo Novemba 2020 jijini Kigali. Ilianza dirisha la pili kwa kupoteza 69-51 mikononi mwa Senegal, ikashangaza mabingwa wa taji 11 ya AfroBasket Angola 74-73 kabla ya kupoteza 71-44 dhidi ya Msumbiji.

Kwa kukamilisha kundi hilo la B katika nafasi ya tatu, nyuma ya Senegal na Angola, Kenya ilifuzu kushiriki AfroBasket kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 28.

Msumbiji, ambayo ilikuwa kwenye AfroBasket mara 10 mfululizo, ilivuta mkia baada ya kushinda mchuano mmoja pekee na ikafungiwa nje ya dimba hilo kwa mara ya kwanza tangu 1999.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa sharubati tamu ya tende, maziwa na njugu...

Motisha Arsenal baada ya kiungo tegemeo Thomas Partey...