Tarehe ya refarenda kujulikana mwezi Machi

Na JUSTUS OCHIENG

TAREHE ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi inayolenga kurekebisha Katiba kupitia Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) 2020 itatangazwa mwishoni mwa Machi.

Hayo yanajiri huku Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya akisema kuwa Bunge limeanza mchakato wa kupitisha mswada huo baada ya kuidhinishwa na zaidi ya mabunge 40 ya kaunti.

“Kuna kamati maalumu ambayo imeundwa na maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti kushughulikia mswada huo. Kamati hiyo itapokea vyeti vya kuidhinisha Mswada wa BBI kutoka kwa mabunge ya kaunti. Tukipata vyeti 24, mchakato wa kupitisha mswada huo utaanza mara moja,” akasema Bw Kimunya.

Kiongozi huyo wa Wengi alisema kuwa mswada huo utawasilishwa rasmi Bungeni wiki ijayo.

Mwenyekiti mwenza wa Sekretariati ya BBI Junet Mohamed alisema kuwa wanatarajia kwamba Bunge litaidhinisha mswada huo katika muda wa wiki tatu.

“Baada ya kuidhinishwa na Bunge, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itatakiwa kutangaza tarehe ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi,” akasema Bw Mohamed.

Mswada unaotoa mwongozo kuhusu namna ya kufanywa kwa kura ya maamuzi Alhamisi ulisomwa kwa mara ya pili katika Bunge la Kitaifa.

“Mswada huo unatarajiwa kuwasilishwa tena Bungeni hivi karibuni ili kusomwa kwa mara ya tatu na nina imani kwamba wabunge wataupitisha bila kuwepo kwa vizuizi,” akasema Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Emmanuel Wangwe.

Bw Kimunya alisema kuwa wanatarajia kuwa asilimia 80 ya Wakenya watapitisha Mswada wa BBI.

“Waliokuwa wakieneza madai ya kupotosha kuhusu BBI sasa wanajua kuwa wamekuwa wakifanya kazi ya bure,” akasema.

“Wamekuwa wakipoteza muda wao kuzunguka kote nchini wakihadaa Wakenya. Sasa ni jukumu la wananchi kuidhinisha mswada huu baada ya ukweli kujitenga na uongo,” akaongezea.

Mwenyekiti mwenza wa sekretariati ya BBI Dennis Waweru ameitaka mahakama kuweka maslahi ya nchi mbele na kutupilia mbali kesi zilizowasilishwa kortini kupinga BBI.

Alisema kuwa Wakenya wanafaa kupewa fursa ya kuamua ikiwa watapitisha au kukataa mswada huo.

“Treni ya BBI tayari imeondoka na kama unataka kuabiri chukua pikipiki au teksi uende utungojee kwenye kituo kilicho mbele. Ukitufuata na wilibaro utaachwa na treni,” akasema Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Mohamed.

Mwakilishi wa Wanawake wa Laikipia Cate Waruguru alisema kuwa watafanya kampeni kali ya kupigia debe BBI.

Aliyekuwa mbunge wa Kibwezi Kalembe Ndile alimtaka Naibu wa Rais William Ruto kubadili msimamo wake na kuunga mkono BBI.

“Naibu wa Rais abadilishe msimamo wake mgumu na aache kuwa na roho yake ya ujanja. Ajue Wakenya wamejanjaruka sasa,” akasema Bw Ndile.

Katibu wa Vuguvugu la Wabunge wa Jubilee Adan Keynan, Maoka Maore (Naibu Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa) na Jimmy Angwenyi (Naibu Kiongozi wa Wengi) walisema kuwa Mswada wa BBI utapitishwa na wabunge na maseneta bila kizuizi.

Mbunge wa Nyeri Mjini Wambugu Ngunjiri alisema kuwa kupitishwa kwa Mswada wa BBI katika eneo la Mlima Kenya ni ishara kwamba Rais Uhuru Kenyatta angali anadhibiti siasa za eneo hilo.

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU

Kwani kuliendaje?