Kichwa kinauma

WANDERI KAMAU na JUSTUS OCHIENG

CHAMA cha ODM Alhamisi kiliongeza muda wa kuwasilisha maombi ya kuwania urais kwa tiketi yake katika uchaguzi wa mwaka wa 2022 hadi Machi 31, hatua ambayo imeibua maswali kuhusu mikakati ya kisiasa ya kiongozi wake, Bw Raila Odinga.

Awali, chama hicho kilikuwa kimetangaza leo kama siku ya mwisho ya kupokea maombi hayo, lakini kikabadilisha uamuzi huo ghafla hapo jana.

Kufikia jana, ni Gavana Hassan Joho wa Mombasa pekee aliyekuwa ametuma maombi hayo na kulipa ada ya Sh1 milioni kama inavyohitajika na Baraza la Kitaifa la Uchaguzi la Chama (NEB).

Ikizingatiwa wengi walitarajia Bw Odinga kuwasilisha stakabadhi hizo, imeibuka kuwa kiongozi huyo anafuatilia kwa kina mienendo ya washindani wake wa kisiasa uchaguzi huo unapokaribia.

Wadadisi wa siasa wanasema kwa kutowasilisha maombi yake jana, Bw Odinga anawatazama kwa kina washindani wake ambao wametangaza azma ya kuwania urais.

Kufikia sasa, vigogo wa kisiasa ambao wametangaza azma zao kuwania urais mwaka ujao ni Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi (ANC), Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Seneta Gideon Moi (Baringo) ambaye pia ndiye kiongozi wa Kanu.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo Jumatano, mdadisi wa siasa Prof Macharia Munene, alisema lengo kuu la Bw Odinga ni “kutazama mienendo ya vigogo hao kisiasa kwani mielekeo yao itamwathiri moja kwa moja”.

“Bw Odinga anaepuka kosa la kuweka wazi mpango wake kuhusu 2022. Anawatazama kwa kina washindani wake, hasa Dkt Ruto baada ya matokeo ya Mpango wa Maridhiano (BBI) katika mabunge ya kaunti,” akasema Prof Munene.

Kufikia sasa, Dkt Ruto na washirika wake wamebaki kimya tangu matokeo hayo yalipotangazwa.

Licha ya kuwa kawaida yake kutoa hisia zake kuhusu mielekeo ya kisiasa nchini, Dkt Ruto amebaki kimya, hata kwenye mitandao ya kijamii.

Wadadisi pia wanasema Bw Odinga anajaribu kukwepa lawama za Mabw Kalonzo, Mudavadi na Wetang’ula, ambao wamekuwa wakimtaja kama “msaliti na mwongo” kwa kutoheshimu muafaka wa Muungano wa NASA mnamo 2017.

Kulingana na mwafaka huo, Bw Odinga alikuwa ameahidi kutowania tena urais ikiwa wangeshindwa katika uchaguzi huo, na badala yake kumuunga mkono mmoja wa vigogo hao 2022.

Hata hivyo, watatu hao wamekuwa wakimtaja Bw Odinga kama mwanasiasa asiyeaminika, baada ya kubuni handisheki na Rais Uhuru Kenyatta bila kuwaarifu.

“Bila shaka, lawama za vigogo hao watatu zinaendelea kumpaka tope Bw Odinga, hata ikiwa hajaweka wazi ikiwa atawania urais au la. Uamuzi huo utapunguza lawama zao kwani wataendelea kuwa gizani kuhusu azma yake. Ikiwa angeweka wazi azma hiyo, basi hilo lingewapa nafasi ya kumsawiri Bw Odinga kama msaliti,” akasema Bw Javas Bigambo, ambaye ni mdadisi wa siasa kwenye mahojiano jana.

Licha ya hayo, ODM imepuuzilia mbali hisia hizo.

Mwenyekiti wa NEB, Bi Catherine Mumma, alisema uamuzi wa chama hicho ulichochewa na chaguzi ndogo zinazotarajiwa kufanyika katika maeneobunge ya Matungu na Kabuchai hapo Alhamisi ijayo.

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ODM, Bw Junet Mohamed, alisema uamuzi huo unalenga kutoa nafasi kwa utekelezaji wa BBI.

“Ni majuzi tu ambapo mabunge yalipitisha BBI. Hatutaki kuchanganya mambo,” akasema.

Habari zinazohusiana na hii

UHURU AMTULIZA RAILA

Wababaisha ‘Baba’

ODM: Raila anachezwa

Kingi amzima Raila

Raila akausha marafiki