• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Faki ataka nakala za BBI kwa Kiswahili

Faki ataka nakala za BBI kwa Kiswahili

Na WACHIRA MWANGI

SENETA wa Mombasa Mohamed Faki ameitaka serikali ichapishe nakala ya mswada wa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) kwa lugha ya Kiswahili ambayo itaeleweka na Wakenya wengi.

Baada ya kaunti 40 kupitisha mswada huo, Bw Faki alisema sasa kibarua kilichoko ni kwa Wakenya kuisoma ripoti hiyo kwa undani na kuelewa yaliyomo kabla ya kufanya uamuzi kwenye kura ya maamuzi. Alisisitiza kuwa wengi wataelewa BBI iwapo nakala hizo zitachapishwa kwa Kiswahili.

Seneta huyo alikuwa akizungumza katika hoteli moja mjini Mombasa wakati wa uzinduzi wa matandiko maalum ya mezani yenye nembo ya Taifa Leo yatakayotumika kwenye mikahawa na hoteli mbalimbali Pwani.

Aidha, mwanasiasa huyo aliirai Kampuni ya Habari ya Nation Media Group ambayo inamiliki gazeti hili kuchapisha nakala za BBI kwa lugha ya Kiswahili ili Wakenya wapate nafasi ya kusoma mswada huo wanaponunua gazeti hilo.

Kauli yake ilitokana na uwezekano kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka huenda isiwe na bajeti ya kugharimia uchapishaji wa mswada huo kwa lugha ya Kiswahili.

“Tunashukuru kwamba tuna Shirika la Nation ambalo limetupa nafasi ya kusoma habari kwa lugha rahisi ambayo tunaielewa kupitia gazeti la Taifa Leo. Kwa kuwa tuko katika mwaka wa siasa mchapishe nakala za BBI kwa lugha ya Kiswahili ili wasomaji waelewe masuala yaliyomo na kujiamulia,” akasema Bw Faki.

Kiongozi huyo alimiminia sifa gazeti hili akisema limesaidia katika makuzi ya lugha na masomo mengine kwa wanafunzi shuleni kupitia mradi wa kuchapisha majaribio ya mitihani magazetini almaarufu NiE

“Mombasa ndicho kitovu cha Kiswahili na uzinduzi huu ni hidaya kwetu. Kupitia matandiko haya tutaweza kusoma Taifa Leo na kufahamu matukio yanayojiri sehemu mbalimbali,” akaongeza

Afisa Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mauzo wa NMG Clifford Machoka naye aliwataka wakazi wa Pwani na Wakenya wote waendelee kusoma gazeti la Taifa Leo ambalo linalotoa habari kwa lugha inayoeleweka na watu wote.

“Tunawashukuru sana kwa kusoma Taifa Leo kila mara. Nyie ndio mashabiki nambari moja wa wa gazeti na tunafanya juu chini kuhakikisha kwamba mnapata habari moto moto. Pia tungependa kusikiza maoni yenu kuhusu masuala tunayofaa kuyakumbatia ili kuboresha zaidi gazeti hili. Muwe huru kuzungumza nasi kila wakati,” akasihi Bw Machoka.

Aliongeza kwamba gazeti hili litasambazwa zaidi katika eneo hilo na maeneo mengine nchini ili kuwafikia wananchi, lengo kuu likiwa kuongeza ufasaha katika lugha ya Kiswahili.

You can share this post!

Kampeni za Matungu zaingia hatua ya lala-salama

MATHEKA: BBI inafaidi wanasiasa pekee mzigo ukiwa kwa raia