• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:33 AM
TAHARIRI: Serikali isambaze nakala za Kiswahili

TAHARIRI: Serikali isambaze nakala za Kiswahili

KITENGO CHA UHARIRI

KWENYE mafunzo ya kidini, kuna kisa kilichosimuliwa kumhusu mtu mwerevu.

Jamaa huyo, inasemekana alijenga nyumba yake juu ya mwamba. Hata mawimbi na mafuriko yalipofika, hayakuifikia nyumba hiyo.

Mtu huyo alitambua kwamba kuna nyakati nzuri na baadaye huja nyakati ambapo inabidi mwanadamu akumbane na misukosuko. Njia bora ya kukabili hali hiyo ni kujiandaa kwa kuweka imara msingi.

Mswada wa marekebisho ya Katiba (2020) maarufu kama BBI sasa umefika mbele ya Bunge la Kitaifa. Ingawa jana Kaunti ya Nandi ilijiunga na Baringo kuukataa, uamuzi huo ni wa kidemokrasia tu na hautaathiri mchakato wa kuujadili mswada bungeni. Iwapo Bunge la Kitaifa na la Seneti yatauidhinisha, itakuwa zamu yaTume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutunga swali ambalo Wakenya watapewa ili kuamua kama ni NDIO au LA kwenye referenda.

Kamati Simamizi ya BBI imetangaza kwamba Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga wanapanga kuanza kampeni zakuvumisha BBI kote nchini kuanzia Machi mosi. Uvumishaji huo hautakuwa na ushawishi wowote kwa mamilioni ya Wakenya watakaoweza kushawishiwa kiurahisi kuikataa BBI kwa kuwa watakuwa hawajaisoma na kuelewa yaliyomo ndani.

Mikutano hiyo, iwapo itaendeshwa kama ilivyo kawaida ya kampeni humu nchini, itageuzwa jukwaa la kuwakashifu waliokataa BBI kwenye mabunge ya kaunti, bila ya kuwaeleza wananchi ni kwa nini wanapaswa kuipitisha.

Kuanza kusema jinsi Naibu Rais na wafuasi wake walivyokataa au kurindima ngoma ya 2022 bila kumfahamisha Mkenya kumeandikwa nini, itakuwa sawa na yule mtu aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. Maji na mawimbi yalipokuja, yaliisomba.

Inawezekana kwamba Mswada wa BBI una mambo mazuri kwa nchi. Mfano ni kuifanyia marekebisho sheria ya mwaka 2003 inayohusu kesi za Ufisadi. Ndani ya BBI, inapendekezwa kuwa kesi za ufisadi zisikizwe na kuamuliwa ndani ya miezi sita. Watakaofichua wafisadi, kesi zikiisha na pesa ya umma irudishwe, watapewa mgao wa pesa hizo kama njia ya kuwapa moyo wengine wasifishe ufisadi.

Haya hayawezi kujulikana na mwananchi iwapo kampeni hazitazingatia kuwafunza yaliyomo. Muhimu zaidi, nakala za BBI zisambazwe kwa lugha ya Kiswahili.

Kwa njia hiyo, hata wakongwe vijijini watajisomea na kuelewa kama BBI ni ya manufaa ua la, badala ya kungoja kusikiza propaganda.

You can share this post!

OMAUYA: Kauli ya Ruto: ‘nichukie ila swara tutamla hadi...

KIKOLEZO: Mbwembwe za showbiz