• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
KIKOLEZO: Mbwembwe za showbiz

KIKOLEZO: Mbwembwe za showbiz

Na THOMAS MATIKO

OKTOBA 2020 mvunja mbavu Eric Omondi aliwashangaza maelfu ya mashabiki wake na mwonekano wake mpya.

Kwa miaka mingi, wengi walimzoea kuwa na mwili mdogo uliokondeana, ila aliwaacha wengi kwa mshangao baada ya kuongezeka mwili ghafla na kuwa na misuli.

Katika kipindi cha mwaka mmoja, alikuwa akifanya mazoezi chini ya maji na kuweza kuongeza zaidi ya kilo 26 ya misuli. Sababu zake kuingia gym na kujipatia mwonekano mpya hazikutokana na kwamba alipania kubadilika, hapana. Eric alifanya jambo hilo kwa sababu moja tu, nayo ni burudani.

“Nilikuwa na mpango wa kufungua studio kufikia mwisho wa mwaka jana na nilitaka wakati wa uzinduzi nije tofauti na hapo ndipo wazo la kujenga mwili wangu likanijia. Nilijua wengi wangeshangaa kwa sababu kwa miaka mingi walinifahamu kuwa mwembamba. Huko kuingia gym nilifanya kwa sababu ya showbiz,” Eric aliniambia kwenye mahojiano.

Tukio la Eric sio geni sana kule Hollywood. Wapo waigizaji wengi ambao wamelazimika kubadilisha mionekano yao ili kutosheleza uhusika wa filamu fulani. Wengi wameishia gym na mazoezini kupungua au kuongeza ilimradi waweze kupata mwonekano wa uhusika unaotakiwa kutoa burudani.

CHRIS HEMSWORTH

(Thor 2011)

Chris alipopata shavu la kuigiza Thor, alitakiwa kuwa pandikizi la mtu ili kuendana ha uhusika. Thor anaaminika kuwa mmoja wa miungu waliowahi kuwepo. Ni miungu wa radi na kimbunga. Anasemekana kuwa na nguvu za ajabu na ni mkubwa ajabu.

Hivyo ili kutosheleza uhusika huu, mwigizaji huyu alitakiwa kuongeza kilo kadhaa za misuli. Alianza mazoezi makali yaliyomwezesha kuongeza kilo tisa. Kando na unyanyuaji wa vyuma na mazoezi mengine kama hayo, alikula sana vyakula vya protini na matunda jambo lililomwezesha kuvimba. Chris alivimba kiasi cha kuwa nguo zake nyingi zilimkataa. Mwonekano huo ndio alioudumisha kwenye filamu zilizofuatia Thor:Ragnorak na Avengers:Endgame.

BRADLEY COOPER

(The A-Team Series)

Ili kuvalia uhusika wa Templeton ‘Faceman’ Peck kwenye filamu ya The A-team, Bradley alitakiwa kubadilisha mwonekano wake ili kuendana na uhusika. Uhusika wake ulikuwa wa mwanajeshi wa zamani na kutokana na mwili wake kuwa mdogo wakati huo akipewa kazi, alitakiwa kuunga ili aendane na uhusika.

Kutokana na hali hiyo, aliacha kula sukari, chumvi, vyakula vya unga wa ngano na mikate. Hali hii ikamwezesha kupoteza kitambi kidogo alichokuwa nacho. Pia alikesha gym kila siku kwa muda wa saa mbili akifanya mazoezi ya ‘cardio’ mara tatu, mazoezi ya unyanyuaji vyuma mara mbili na zoezi moja la tumbo kwa dakika 10. Ilibidi aache pombe pia ili kupunguza mafuta mwilini.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali isambaze nakala za Kiswahili

DOMO KAYA: Leo hii kajifanya mbogo!