• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 5:29 PM
Mfanyabiashara aliuawa kinyama – Uchunguzi

Mfanyabiashara aliuawa kinyama – Uchunguzi

Na MARY WAMBUI

UCHUNGUZI wa maiti ya mfanyabiashara Caroline Wanjiku Maina umefichua kuwa alifariki kutokana na majeraha mabaya utosini na mgongoni.

Familia ya marehemu pia ilisema uchunguzi huo ulidhihirisha kwamba marehemu alijeruhiwa vibaya sana kwenye makalio.

“Tumeelezwa kama familia na kuridhika na uchunguzi huo. Alifariki kutokana na majeraha kichwani baada ya kugongwa utosini na mgongoni,” akasema dadaye mkubwa Rose Thongori.

“Pia alikuwa na majeraha mabaya sana makalioni na gololi za macho yake hazikung’olewa jinsi ilivyokuwa ikidaiwa licha ya kuwa mwili ulikuwa umeanza kuoza,” akaongeza.

Marehemu atazikwa leo katika kijiji cha Kangari, Murang’a na amewaacha watoto wawili. Bi Wanjiku aliyekuwa mfanyakazi wa benki ya Co-operative ya Embu alihadaiwa na kutekwa nyara baada ya kuahidiwa kwamba angeongezewa akiba yake ya Sh350,000 zilizokuwa katika shirika la akiba na mikopo la Stima (Sacco).

Alitoa hela hizo kwenye tawi la benki hiyo katika jengo la Stima Plaza mnamo Februari 12 kabla kuondoka ili akutane na mmoja wa waliodaiwa kumteka nyara na aliyekuwa mpenziwe katika mtaa wa Ngara, Nairobi.

Mwili wake baadaye ulipatikana umetupwa katika Shule ya Msingi ya Gatina, mtaani Kawangware siku iliyofuatia huku washukiwa wanne wakitiwa mbaroni. Wanne hao ni Edwin Otieno Odiwuor, Stevenson Oduor Ouma, Samwel Okoth Adinda na Mercy Gitiri Mongo ambaye alikuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la NYS Kaunti ya Embu.

You can share this post!

DOMO KAYA: Leo hii kajifanya mbogo!

Mbunge awahimiza vijana na wafanyabiashara Ruiru kuunda...