Jinsi serikali inavyozima kampeni ya wilibaro ya Ruto

Na BENSON MATHEKA

SERIKALI imeweka mikakati ya kuzima kampeni ya “Kazi ni Kazi” ambayo Naibu Rais William Ruto amekuwa akitumia katika kampeni yake ya kuwezesha vijana kwa kuwapa wilibaro na vifaa vingine kuanzisha biashara.

Kupitia mpango wa kusaidia vijana kuanzisha biashara na kubuni nafasi za kazi, serikali imeanzisha shindano linalofahamika kama “Mbele Na Biz” ambapo vijana 750 watanufaika na ufadhili wa Sh15 bilioni.

Shindano hilo lilianzishwa na Rais Uhuru Kenyatta katika uwanja wa michezo wa Kasarani Jumatano ambapo aliwasihi waunge mswada wa kubadilisha katiba akisema utaweka mazingira mazuri ya kuwawezesha kufanya biashara.

Kuvumishwa kwa shindano hili wakati wa kampeni za mageuzi ya katiba kumechukuliwa na wadadisi kuwa juhudi za kuzima kampeni ya Dkt Ruto ya kusaidia vijana kutoka familia masikini kujijenga kiuchumi kupitia vuguvugu la hasla.

“Ni mpango wa kubomoa kampeni ya Dkt Ruto ya kuwapa vijana wilibaro na mikokoteni. Serikali inamwaga mabilioni kuwaonyesha vijana kwamba wanastahili kazi za maana kuliko kuendesha wilibaro na kuvuta mikokoteni,” asem mdadasi wa masuala ya mikakati ya utawala, Evan Oloo.

Dkt Ruto amekuwa akikosoa mageuzi ya kikatiba akisema anachojali ni kusaidia vijana kujijenga kiuchumi.

Shindano hilo linaendeshwa chini ya mradi wa kutoa ajira kwa vijana wa Kenya Youth Employment Opportunities Project (KYEOP).

Kulingana na Waziri msaidizi (CAS) katika Wizara ya ICT, Ubunifu na Masuala ya Vijana Bi Nadia Mohammed, vijana wengine 1,500 watapatiwa mafunzo ya kuandaa mipango ya biashara chini ya KYEOP, ambao ni mpango wa serikali ya Kenya na Benki ya Dunia.

Bi Nadia alisema KYEOP, ni mpango wa kulinda jamii na kuwawezesha vijana ambao unatekelezwa kwa miaka mitano (2016-2021) kuongeza nafasi za ajira na mapato kwa vijana wanaolengwa walio na umri wa kati ya miaka 18 na 29.

Bi Nadia alieleza kwamba wale watakaonufaika na ufadhili wa Sh15 billioni kutoka Benki ya Dunia, lazima wawe wamesoma hadi kidato cha nne.

Alisema kwamba mradi huo unatekelezwa katika kaunti 17 za Mombasa, Kilifi, Nairobi, Nakuru, Kiambu, Nyandarua, Mandera, Turkana, Wajir, Bungoma, Kakamega, Kwale, Kisumu, Kisii, Machakos, Kitui na Migori.

Waziri huyo msaidizi alisema kwamba utekelezaji wa mradi huo unahusu mashirika manne ya serikali.

Chini ya mpango huu, Nadia alieleza, vijana 250 walio na mipango ya biashara au biashara zilizo na uwezo wa kutoa nafasi nyingi za kazi watapokea kila mmoja Sh 3.6 milioni na wengine 500 watapokea Sh 900,000 kila mmoja. Mojawapo ya shughuli za mpango wa KYEOP, alisema Bi Nadia, ni kuwapa mafunzo na tajiriba ya maeneo ya kazi, vijana, ambayo inatekelezwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Taifa Kuhusu mafunzo (NITA) na wizara ya ICT, Ubuni na Masuala ua vijana.

Aliongeza kuwa hii inahusu mafunzo kwa vijana wapate ujuzi chini ya usimamizi wa NITA ambapo wanatuma maombi ya kupata mafunzo.

Nafasi za mafunzo zitatangazwa kupitia magazeti, redio na runinga.

Bi Nadia alisema kwamba mafunzo katika kundi hili yatatolewa kwa njia mbili, kufunzwa maarifa ya kazi kwa miezi mitano na mafunzo ya kawaida madarasani kwa miezi miwili na kisha miezi mingine mitatu ya kujifunza kazi halisi kwenye mazingira ya viwanda.

Bi Nadia alisema watakaopata mafunzo ya taaluma mbalimbali watakuwa wakipokea marupurupu ya uchukuzi ya Sh 6000 kila mmoja wakihudhuria asilimia 80 ya mafunzo na pia watafunzu kuomba pesa za kuanzisha biashara za taaluma watakazofunzwa au nyingine watakazopenda. Waziri huyo msaidizi alisema kupitia kitengo cha pili cha kubuni nafasi za ajira ambacho kinashirikishwa na mashirika madogo ya kifedha (MSEA) yakisaidiwa na wizara ya ICT, Ubunifu na Masuala ya Vijana, vijana watafaidika na ruzuku ndogo na shindano la Mpango wa Biashara (BPC) litakalofahamika “Mbele Na Biz”.

Bi Nadia aliongeza kuwa ruzuku hizo ndogo zinalenga vijana 30,000 wanaoendesha biashara ndogo ndogo au walio na nia ya kuanzisha biashara mpya na hawana mtaji.

Vijana hao, alifichua, watapokea ruzuku ya Sh40, 000 kwa awamu mbili kwa wale watasajiliwa na kufunzu mtihani wa ufahamu wa Masuala ya Biashara (EAT) ambao husaidia kufahamu ikiwa wanaotuma maombi wanaelewa biashara wanazonuia kuanzisha.

Waziri msaidizi Nadia alisema kwamba shindano la ‘MbeleNaBiz’ linanuiwa kubuni biashara mpya zinazosimamiwa na vijana na kupanua zilizopo kwa kuwapa ufadhili na/ au mafunzo kuhusu biashara. Alifichua kwamba shindano hilo litaanza wiki hii katika uwanja wa michezo wa Kasarani na washindi katika vitengo vinne vya shindano hilo watapatiwa zawadi.

Habari zinazohusiana na hii

BBI YAINGIA ICU

Kwani kuliendaje?