• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
Liverpool hawatajishughulisha sana sokoni mwishoni mwa msimu huu wa 2020 hadi 21 – Klopp

Liverpool hawatajishughulisha sana sokoni mwishoni mwa msimu huu wa 2020 hadi 21 – Klopp

Na MASHIRIKA

KOCHA Jurgen Klopp amesema kwamba kikosi chake cha Liverpool hakitahitaji kusajili idadi kubwa ya wanasoka kwa minajili ya kujisuka upya mwishoni mwa msimu huu.

Baada ya kupoteza mechi nne mfululizo kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa kipute hicho kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita huku pengo la pointi 19 likitamalaki kati yao na viongozi Manchester City.

Jumla ya wanasoka 12 wa kikosi cha Liverpool wana umri wa zaidi ya miaka 28, wakiwemo masogora tisa tegemeo wa kikosi cha kwanza.

“Sidhani kuna haja ya kujishughulisha sana sokoni kwa nia ya kujisuka upya. Kikosi cha mwaka huu hakikupata fursa ya kucheza pamoja kwa muda mrefu. Zaidi ya kurekebisha hilo, pia yatahitajika mabadiliko machache ambayo yatafanyika,” akasema Klopp, 53.

Liverpool wameshinda mechi mbili pekee kutokana na 11 zilizopita ligini na walibanduliwa kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA na League Cup msimu huu.

Ingawa hivyo, Liverpool almaarufu The Reds wanajivunia msimu wa kuridhisha kwenye kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) ambapo kwa sasa wanajiandaa kurudiana na RB Leipzig ya Ujerumani baada ya kusajili ushindi wa 2-0 kwenye raundi ya kwanza ya hatua ya 16-bora ya kivumbi hicho.

Kiungo na nahodha Jordan Henderson ndiye mchezaji wa hivi karibuni zaidi kuunga orodha ya wanasoka wanaouguza majeraha kambini mwa Liverpool na sogora huyo raia wa Uingereza anatarajiwa kusalia mkekani kwa kipindi cha wiki 10 zijazo baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye kinena.

Akihojiwa na wanahabari mnamo Ijumaa baada ya kuongoza kikosi kufanya mazoezi kwa minajili ya gozi la EPL dhidi ya Sheffield United mnamo Februari 28, Klopp alisema kubwa zaidi katika malengo ya Liverpool kwa sasa ni kukamilisha kampeni za EPL muhula huu katika mduara wa nne-bora na kufuzu kwa soka ya UEFA msimu ujao wa 2021-22.

“Kufikia malengo hayo ni hatua kubwa ikizingatiwa ubovu wa hali inayotukabili kwa sasa. Majeraha yametulemaza na kikosi kinapitia changamoto tele,” akasema kocha huyo raia wa Ujerumani ambaye pia amewahi kuwatia makali masogora wa Borussia Dortmund nchini Ujerumani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Fowadi Antonio Michail wa West Ham afichua mpango wa kutema...

Ruto kufukuzwa nyumbani