• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Man-Utd wapewa AC Milan, Arsenal kuvaana na Olympiakos huku Spurs wakionana na Zagreb kwenye hatua ya16-bora Europa League

Man-Utd wapewa AC Milan, Arsenal kuvaana na Olympiakos huku Spurs wakionana na Zagreb kwenye hatua ya16-bora Europa League

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United watavaana na mabingwa mara saba wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), AC Milan, kwenye hatua ya 16-bora ya Europa League msimu huu.

Ni kivumbi kinachotarajiwa kukutanisha kigogo Zlatan Ibrahimovic wa AC Milan na waajiri wake wa zamani, Man-United ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 49.

Kwa upande wao, AC Milan pia wanashikilia nafasi ya pili kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa alama 49, nne nyuma ya viongozi Inter Milan ya kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte.

AC Milan hawajawahi kushinda taji lolote la Europa League. Mara ya mwisho kwa Man-United kujivunia ufalme wa Europa League ni 2017 chini ya kocha raia wa Uholanzi, Louis van Gaal.

Arsenal waliokuwa wanafainali wa 2019, wamepangwa kuchuana na Olympiakos ya Ugiriki iliyowabandua kwenye hatua ya 32-bora mnamo 2020.

Chini ya kocha Jose Mourinho, Tottenham Hotspur wamepewa miamba wa soka ya Croatia, Dinamo Zagreb huku Rangers inayoshiriki Ligi Kuu ya Scotland chini ya kocha Steven Gerrard ambaye ni kiungo na nahodha wa zamani wa Liverpool, wakitiwa zizi moja na Slavia Prague. Slavia ambao ni wapambe wa soka katika Jamhuri ya Czech, waliwadengua Leicester ya kocha Brendan Rodgers mnamo Februari 25 uwanjani King Power.

Mechi za hatua ya 16-bora kwenye Europa League msimu huu zimeratibiwa kupigwa kati ya Machi 11 na 18, 2021.

Ibrahimovic ambaye kwa sasa anauguza jeraha, aanatazamiwa kushiriki mechi ya mkondo wa pili dhidi ya Man-United uwanjani Old Trafford. Mechi hiyo itakuwa ya 13 kuwahi kukutanisha AC Milan na Man-United katika soka ya bara Ulaya. Mechi zote 12 za awali ambazo zimewahi kuwakutanisha AC Milan na Man-United zimekuwa kwenye soka ya UEFA.

Rangers waliobandua Royal Antwerp ya Ubelgiji kwa jumla ya mabao 9-5 kwenye raundi ya 32-bora, walifuzu kwa hatua ya 16-bora kwa msimu wa pili mfululizo mwaka huu. Mechi kati yao na Slavia itakuwa ya kwanza kuwahi kuwakutanisha.

Dinamo Zagreb ambao watakuwa wenyeji wa mchuano wa mkondo wa kwanza dhidi ya Tottenham, wamepoteza jumla ya mechi tisa kati ya 10 zilizopita dhidi ya vikosi vya soka ya Uingereza katika mechi za bara Ulaya. Kikosi hicho kilipepeta Arsenal 2-1 kwenye hatua ya makundi ya UEFA mnamo 2015.

Arsenal waliwahi kubanduliwa na kikosi kimoja mara mbili mfululizo kwenye soka ya bara Ulaya mnamo 2014 baada ya kuzidiwa maarifa na miamba wa soka ya Ujerumani na wafalme wa Kombe la Dunia, Bayern Munich.

Vikosi vitakavyonogesha hatua ya 16-bora ya Europa League vina hadi Jumatatu ya Machi 1, 2021 kuripoti masuala na changamoto zozote za usafiri kwa minajili ya michuano yao kabla ya maamuzi kuhusu mahali ambapo mechi hizo zitasakatiwa kuafikiwa.

DROO YA HATUA YA 16-BORA YA EUROPA LEAGUE:

Ajax na BSC Young Boys

Dynamo Kiev na Villarreal

AS Roma na Shakhtar Donetsk

Olympiakos na Arsenal

Dinamo Zagreb na Tottenham

Manchester United na AC Milan

Slavia Prague na Rangers

Granada na Molde

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Hofu maambukizi ya Covid yakianza kuongezeka tena

Sihitaji BBI kuingia Ikulu, Raila asisitiza