TAHARIRI: Dawa ya tatizo la michezo ni ufadhili

KITENGO CHA UHARIRI

MBALI na riadha, mchezo mwingine ambao Kenya ina uwezo wa kutamba pakubwa kimataifa ni ule wa vikapu vya wanaume iwapo mikakati madhubuti itawekwa na wadau.

Wanavikapu wa Kenya Morans sasa wametiwa katika orodha ya vikosi vitakavyoshiriki mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2023 nchini Japan, Indonesia na Ufilipino.

Hii ni baada ya timu hiyo ya kocha Liz Mills kuwa miongoni mwa vikosi 16 ambavyo tayari vimefuzu kwa fainali za Fiba Afro-Basket zitakazofanyika jijini Kigali, Rwanda mnamo Agosti 24-Septemba 5, 2021.

Japo Morans watashiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza tangu 1993, changamoto za wazi zilizodhihirika katika kampeni zao ni ukosefu wa mpangilio wa kufanikisha maandalizi ya mapema kwa minajili ya michuano hiyo ya kufuzu.

Tatizo hili limekuwa sugu si kwa mchezo wa vikapu pekee, bali hata katika fani nyinginezo za michezo kama vile voliboli, soka, raga, riadha na magongo. Zaidi ya hazina ya fedha kwa michezo, ambayo kwa kweli ni hafifu sana, ipo haja kwa serikali kubuni mikakati madhubuti zaidi ya kufadhili mchezo huu wa vikapu.

Mojawapo ya mambo yanayofaa kuangaliwa kwa undani kabisa ni mgao ambao serikali, kupitia Shirikisho la Vikapu la Kenya (KBF), hutengea kikosi hiki kwa ajili ya mapambano ya kimataifa ya sampuli hiyo. Ifahamike kuwa sekta ya michezo ni mojawapo ya vitengo vinavyoweza kusaidia serikali kupunguza ukosefu wa nafasi za ajira hasa miongoni mwa vijana.

Ingawa hivyo, sekta hiyo inapitia changamoto za kila sampuli zinazohitaji kutafutiwa suluhu haraka iwezekanavyo.

Aidha, pana haja pia ya mashirikisho mbalimbali ya michezo pamoja na wadau katika sekta hiyo kuanza kubuni sera zitakazowezesha timu kujistawisha na kuendesha shughuli zake kwa utaratibu ufaao bila kutegemea serikali pekee.

Ipo haja ya kutungwa kwa sera zitakazovutia mashirika hisani na watu binafsi kudhamini michezo. Aghalabu kinachosababisha wafadhili kutoroka ni sera mbovu na uongozi duni miongoni mwa mashirikisho ya michezo humu nchini.

Itakuwa bora vilevile kuyaiga mataifa yaliyopiga hatua ya maana si katika vikapu tu bali pia katika fani nyinginezo kama vile voliboli ili kupunguza baadhi ya matatizo katika michezo hii inayoanza kuvunia Kenya sifa nzuri.

Uwekezaji wa kutosha ndiyo suluhu pekee ya kudidimia kwa viwango vya mchezo wa vikapu nchini na mingineyo.

Ni fedheha kwa Kenya, kwa mfano, kutofuzu kwa fainali za Afro-Basket kwa kipindi kirefu licha ya kujivunia huduma za wanavikapu shupavu wanaochezea vikosi maarufu vya bara Ulaya. Sharti hali hii ibadilike upesi maadamu mashabiki wa vikapu wangependa kuona fahari pale vijana wa Kenya wanapotamba katika mashindano ya haiba kubwa.

 

Habari zinazohusiana na hii